Carrol Sonie afunguka kwa nini alihama kutoka kwa nyumba ya wazazi wake hivi majuzi

Sonie amesema alikuwa sawa na kuishi katika nyumba ya wazazi wake kwani hakuwa tayari kukaa peke yake.

Muhtasari

•Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 25 alitangaza wazi kwamba ilikuwa mapema mwezi huu ambapo alianza kuishi peke yake.

•Pia alibainisha kwamba alihitaji pia kujikuza na kujifanyia kazi mwenyewe kwa kuishi peke yake.

Image: INSTAGRAM// CAROLINE MUTHONI

Muigizaji na mtayarishaji wa maudhui Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonie amekiri kwamba alihama kutoka kwa wazazi wake hivi majuzi.

Katika mahojiano na Obinna TV, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 25 alitangaza wazi kwamba ilikuwa mapema mwezi huu ambapo alianza kuishi peke yake.

Sonie alisema kuwa amekuwa akiishi na wazazi wake hadi alipopanga nyumba yake mwenyewe kwani hakuwa tayari kuanza kuishi peke yake.  Aidha, aliweka wazi kwamba wazazi wake hawawahi kumpa shinikizo la kuhama nyumba yao.

"Nilihisi kama ni wakati sahihi. Nilikuwa nimepanga kila kitu, nilisema kabla sijahama, nahitaji kukarabati nyumba ya mama yangu, nataka niifanye wakae vizuri kabla sijatoka. Hayo yote yalipofanywa, nilisema kwa sababu tayari nina baraka za mzazi na pamoja na Mungu, sioni maana ya kubaki huko,” Carrol Sonie alisema.

Mama huyo wa binti mmoja pia alibainisha kwamba alihitaji pia kujikuza na kujifanyia kazi mwenyewe kwa kuishi peke yake.

“Wazazi wangu hawajawahi kuniambia nihame. Kwa kweli, wao ndio wazazi wanaonisaidia sana kuwahi kuona. Sikuchujwa,” alisema.

Sonie hata hivyo alilalamika kuwa kuishi peke yake si rahisi sana. Alisema bei ya vitu vya nyumba ilimshtua hadi akahisi kutaka kurudi nyumbani kwa babake.

Pi alifichua kwamba hakubeba chochote kutoka kwa nyumba ya mzazi wake alipokuwa akihama.

“Juzi nilienda kufanya shopping ya nyumba, nilikuwa naskia kurudi kwa babangu. Nilishangaa kumbe vitu ni ghali hivi. Juzi ndo nimefanya shopping ya kwanza kwa nyumba yangu. Nilihama kama wiki tatu zilizopita. Nilikuwa naishi na wazazi,” alisema.

Sonie alibainisha kwamba alikuwa sawa na kuishi katika nyumba ya wazazi wake kwani hakuwa tayari kukaa peke yake.

“Pia sikutaka kujilazimisha kufanya jambo ambalo siwezi kufanya. Unaona sasa naweza kulipa kodi yangu mwenyewe, naweza kununua chochote ninachotaka kujinunulia. Huko nyuma, singeweza. Pia sipendi kutegemea mtu yeyote. Ninapenda kujifanyia mambo, ninapostarehe, nafanya nikiwa tayari,” alisema.

Aidha, alifichua kwamba alimwacha bintiye na wazazi wake kwa muda alipohama.