Zari arejea Uganda kumshawishi mumewe Shakib arudi kwenye ndoa, ajuta kumdhalilisha mtandaoni

"Niko hapa kurekebisha mambo, nilichosema kwenye mtandao sio sawa, nakubali, nataka mume wangu Shakib arudi," Zari alisema.

Muhtasari

•Zari amekiri kuwa sababu ya ziara yake hiyo ni kutaka kurudiana na mumewe Shakib ambaye alitofautiana naye hadharani wiki kadhaa zilizopita.

•Zari alikiri kuwa ilifanya makosa makubwa kutumia mitandao ya kijamii kushughulikia masikitiko yake na Shakib.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti wa Uganda anayeishi Afrika Kusini, Zari Hassan alirejea katika nchi yake ya kuzaliwa mwishoni mwa wiki jana kwa safari ya siku chache.

Akizungumza wakati wa mahojiano ya wikendi, mama huyo mwenye umri wa miaka 43 alikiri kuwa sababu ya ziara yake hiyo ni kutaka kurudiana na mumewe Shakib Cham Lutaaya ambaye alitofautiana naye hadharani wiki kadhaa zilizopita.

Zari alikiri kwamba alifanya makosa kwa kuzungumza vibaya kuhusu mumewe mtandaoni na kulaumu matendo yake kwa masikitiko yaliyomkumba.

"Mambo hutokea. Mungu alituumba ili tufanye makosa. Tunafanya makosa, lakini baadaye unatafakari na kutambua ulivuka mipaka," Zari alisema.

"Mimi ni mwanamke mkaidi. Mimi ni mwanamke anayejitegemea. Mimi ni Zari the BossLady. Lakini, kwa kweli, nilifanya makosa, nilikuwa na madhaiko yangu," aliongeza.

Mama huyo wa watoto watano alikiri kuwa ilifanya makosa makubwa kutumia mitandao ya kijamii kushughulikia masikitiko yake na Shakib.

Aliweka wazi kwamba alifunga safari ya kurudi nchi ya mama yake kimsingi kwa sababu anataka mumewe arudi.

"Niko hapa kurekebisha mambo, nikisema chochote nilichosema kwenye mtandao sio sawa, nakubali, nataka mume wangu Shakib arudi," alisema.

Mwezi uliopita, Zari alizamia kwenye mitandao ya kijamii kumzomea mumewe Shakib na kutishia kumuacha. Hii ilikuwa baada ya Shakib kuonyesha kutilia shaka uhusiano wa  Diamond na mkewe.

Katika kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao wa kijamii, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa mumewe hana uhakika kuhusu ndoa yao na amekuwa akihoji uhusiano kati yake na mzazi mwenzake, Diamond Platnumz.

Zari alisema alilazimika kufanya kipindi cha moja kwa moja ili kueleza wazi kuwa yeye na Diamond hawako kwenye uhusiano wowote wa kimapenzi, ili tu kumhakikishia mumewe kuhusu auaminifu wake katika ndoa yao

“Ngoja niwaambie kitu, Nikitaka kumrudia Diamond naweza kurudi. Ikiwa Diamond anataka kunirudia, anaweza kurudi. Lakini sisi tumemalizana. Sisi tumemalizana kabisa. Simtaki, hanitaki,” Zari alisema Jumapili usiku.

Sosholaiti huyo aliweka wazi kuwa ana mume na mzazi mwenzake pia ana mpenzi.

“Mume wangu hajiamini sana, na hilo linaleta matatizo mengi. Lazima niwe hapa kuelezea. Kweli? Boss lady mzima, inabidi nifanye kipindi chote cha moja kwa moja, ili tu kuthibitisha uhakika kwa mume wangu. Kipindi hiki ni kuthibitisha kitu kwa mume wangu,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kuwa ana sifa zote nzuri na anaweza kuwa na mtu yeyote ambaye anataka kuwa naye.

"Lakini nilimchagua mume wangu, na sijali jinsi nyinyi mnamwona. Ooh, amefilisika, hafai vya kutosha, sijali. Nilimchagua. Nilichagua kuwa naye kama mume wangu, kisha ananiweka katika hili!!,” alisema.

Zari alidokeza kuwa mumewe hana budi kuacha kutokuwa na uhakika kuhusu ndoa yao ikiwa anataka iendelee vyema.