Fahamu matamshi ya Mchungaji Kiengei dhidi ya Pritty Vishy ambayo yamezua kero mtandaoni

Kiengei alikashifu jinsi Pritty Vishy alivyojizolea umaarufu na akakejeli maumbile ya mrembo huyo kutoka Kibera.

Muhtasari

•Katika mahojiano ya hivi majuzi,  mchungaji Kiengei alisikika akizungumza kuhusu uhusiano wa zamani wa Pritty Vishy na Stevo Simple Boy.

•Mtumishi huyo wa Mungu aliendelea zaidi kumdhihaki mwimbaji Stevo Simple Boy pia kwa kuikejeli sauti yake na kumuiga.

Pastor Ben na Pritty Vishy
Image: HISANI

Mtumbuizaji maarufu wa vichekesho vya Kikuyu na kiongozi wa kanisa Benson Gathungu almaarufu Muthee Kiengei anaendelea kupokea ukosoaji mkubwa kutokana na matamshi aliyotoa katika mahojiano ya hivi majuzi dhidi ya mtayarishaji wa maudhui Pritty Vishy na mpenzi wake wa zamani Stevo Simple Boy.

Pritty Vishy, ​​kwa kuungwa mkono na wanamtandao wengine mbalimbali wamejitokeza kumkosoa mchekeshaji huyo na kumtaka awajibike kwa kitendo chake hicho.

Lakini, ni maneno gani haya ya Muthee Kiengei ambayo yamezua hasira nyingi kutoka kwa mtayarishaji maudhui wa miaka 22 na watumiaji wengine wa mtandao?

Katika mahojiano ya hivi majuzi,  mchungaji Kiengei alisikika akizungumza kuhusu uhusiano wa zamani wa Pritty Vishy na Stevo Simple Boy. Alibainisha kuwa kulikuwa na watu wengi ambao walipendezwa na uhusiano wa wapenzi hao wawili, lakini hawakuwahi kujua ni nini Stevo alikuwa akifanywa kupitia na mtayarishaji wa maudhui huyo.

Kiengei aliendelea kukashifu jinsi Pritty Vishy alivyojizolea umaarufu na pia kukejeli maumbile ya mrembo huyo kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera.

“..Huyu amekuja na kumpata Stevo akiwa maarufu, na yeye pia anataka kuwa maarufu. Kupata umaarufu kwake, anataka tumjue na kuwa mnene. Kwa sababu, yeye sio mwimbaji, sio mrembo. Haridhishi,” Kiengei alisema.

Mtumishi huyo wa Mungu  aliendelea zaidi kumdhihaki mwimbaji Stevo Simple Boy pia kwa kuikejeli sauti yake na kumuiga.

Kiengei hata hivyo tayari amenyenyekea na kuomba msamaha kutoka kwa Pritty Vishy kuhusu matamshi aliyotoa dhidi yake.

Jumanne asubuhi, mchekeshaji huyo alizamia kwenye mitandao yake ya kijamii na kuandika ombi la msamaha kwa mpenzi huyo wa zamani wa Stevo Simple Boy na kukiri kuwa alikosea kwa kauli alizotoa dhidi yake.

Kiengei alikiri kwamba alitaja jina la Pritty Vishy kwa njia isiyo sahihi na kwamba alivuka mipaka kwa kauli mbaya alizotoa.

“Prity Vishy, ​​samahani sana na nachukua muda huu kukuomba radhi sana kwa kutaja jina lako kwenye kipindi nilichopitia na kukutaja kimakosa, Pata nafasi moyoni mwako kunisamehe kwa kukuhutubia kwa njia isiyo sahihi, njia mbaya,” Kiengei alisema kupitia Facebook.

Mtumbuizaji huyo ambaye pia ni askofu katika kanisa moja maarufu jijini Nairobi aliahidi kutorudia kosa lilelile na akaendelea kumwalika Vishy kwenye kanisa lake.

"Hii haitatokea siku katika zijazo, naichukulia kama kosa langu, Pole dada yangu na karibu sana JCM CHURCH, KANISA LA WATU WOTE," alisema