"Sitaki ata waniitie bure" Salasya amkataa mwanamke wa Eldoret aliyejitolea kuwa mkewe

“Hizi vitu vya kufuatana na wasichana wa mitandao ya kijamii nimesimamisha rasmi," Salasya amesema.

Muhtasari

•Chebaibai alitumia bango kueleza upendo wake  kwa mbunge huyo kijana na kumjulisha kuhusu kujitolea kwake kuwa mke wake.

•Salasya alionekana kutopenda kukutana naye akibainisha kuwa ameacha rasmi kukutana na wanawake wa mitandao ya kijamii.

Image: HISANI

Mwanasiasa mwenye utata na mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya ameonekana kukataa ombi la ndoa la mwanamke kutoka Eldoret.

Bi Juddie Chebaibai alikuwa ametumia bango kueleza upendo wake  kwa mbunge huyo kijana na kumjulisha kuhusu kujitolea kwake kuwa mke wake.

Chebaibai alibainisha kwamba amekuwa akivutiwa sana na Salasya na hata akaomba usaidizi wa Mbunge Oscar Sudi kumfikia crush huyo wake.

“Nimekuwa nikikutamani sana. Mimi huwa nafuata njia zako na sasa ni wakati wangu wa kukueleza kuwa mimi sijaolewa na moyo wangu unakupenda. Nioe,” Judy aliandika kwenye bango.

Pia alichapisha barua akiwaomba wanamitandao kumsaidia kumfikia mbunge huyo na akatishia kutembea kwa miguu kutoka Eldoret hadi Nairobi ikiwa hamu yake haitatimia.

Katika majibu yake hata hivyo, Salasya alionekana kutopenda kukutana naye akibainisha kuwa ameacha rasmi kukutana na wanawake wa mitandao ya kijamii.

“Hizi vitu vya kufuatana na wasichana wa mitandao ya kijamii nimesimamisha rasmi. Sitaki na sitawahi ata waniitie bure siesi,” Salasya alijibu.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mbunge huyo wa muhula wa kwanza kuhusika katika mabishano makali ya mitandaoni na sosholaiti Huddah Monroe ambaye amekuwa akimvutia kwa muda mrefu.

Wawili hao walionekana kuzozana baada ya kutoelewana kuhusu pesa.