logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Baba akamatwa kwa kumzika mwanawe kwa dakika 90 ili ‘kumuondolea nuksi’ anaposafiri ughaibuni

Inaarifiwa kwamba baba mzazi aliposikia mwanawe amepata visa ya kuenda ughaibuni, alimpeleka kwa mganga ili kufanyiwa matambiko ya kumuondolea mikosi safarini.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Dakia-udaku25 October 2024 - 12:49

Muhtasari


  • Baada ya tambiko, kijana alikimbizwa hospitalini lakini madaktari walisema kuwa amefariki.
  • Mwili wake umewekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi.

Baba mmoja ametiwa mbaroni na polisi baada ya kudaiwa kumzika mwanawe mwenye umri wa miaka 26 kwa saa moja na nusu kama njia moja ya kumuondolea nuksi za safari ya ughaibuni.

Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo la ajabu liliripotiwa kutokea katika mkoa wa Enugu huko Nigeria ambapo kijana huyo baada ya kuzikwa, alipoteza maisha yake.

Inaarifiwa kwamba baba mzazi aliposikia mwanawe amepata visa ya kuenda ughaibuni, alimpeleka kwa mganga ili kufanyiwa matambiko ya kumuondolea mikosi safarini.

Hapo ndipo mganga alipomshauri baba kwamba, ili kuondoa mikosi na nuksi safarini, inabidi kijana huyo afukiwe mchangani kwa saa moja na dakika 30.

Baba alitekeleza agizo la mganga na kwa bahati mbaya mwanawe akafa baada ya kufukiwa kwa kipindi alichoagizwa na mganga.

Afisa wa Uhusiano wa Polisi wa Enugu (PPRO, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao, akisema kuwa mganga, 48, na babake marehemu, 67, wanashtakiwa kwa kula njama na mauaji.

Kauli ya plisi huyo ilieleza kuwa baba huyo alimpeleka mwanawe kwenye madhabahu ya mganga wa kienyeji kwa ajili ya ibada hiyo, ambapo tukio la kifo lilitokea.

“Tukio hilo linadaiwa kutendeka wakati baba alipompeleka mwanawe kwenye madhabahu ya mganga wa kienyeji kwa matambiko yaliyokusudiwa kumtia nguvu kwa hirizi. Hata hivyo, wakati wa tambiko, marehemu alizikwa kwenye jeneza lakini kwa bahati mbaya alifariki katika mchakato huo,” msemaji wa polisi alinukuliwa akisema.

Baada ya tambiko, kijana alikimbizwa hospitalini lakini madaktari walisema kuwa amefariki.

Mwili wake umewekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi.

Kwa mujibu wa polisi, mganga huyo mzawa alikiri kutokea kwa tukio hilo na kutaja matambiko ya awali yanayofanana na hayo, akihusisha kifo hicho na kushindwa kufuata miongozo maalum ya matambiko aliyotoa.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved