"Allah akulinde" Mauzo amuombea bintiye baada ya kudokeza ndoa kuvunjika, Vera avunja kimya

"Niko sawa, na mtoto wangu anaendelea vizuri," Vera Sidika alisema.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, Brown Mauzo alichapisha video ya binti yao, Asia Brown na kuambatanisha na ombi maalum kwake.

•Mwanasoshalaiti Vera Sidika alipohojiwa aliweka wazi kwamba anaendelea vizuri na watoto wao pia walikuwa sawa.

Brown Mauzo, Vera Sidika na binti yao Asia Brown
Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Siku ya Jumatatu, mwimbaji Brian Mutinda almaarufu Brown Mauzo aliibua wasiwasi kuhusu hali ya ndoa yake na Vera Sidika baada ya kufuta picha zote na mwanasosholaiti huyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Isitoshe, msanii huyo kutoka Pwani pia aliacha kumfuatilia mzazi huyo mwenzake kwenye mtandao huo. Haikubainika kwa nini alichukua hatua hiyo lakini  ilikuwa ishara wazi kuwa kuna kitu kinachoendelea kati ya wawili hao.

Wanamitandao wadadisi walifuatilia kwa makini kuona hatua ambayo Vera Sidika angechukua kufuatia hatua hiyo ya kushangaza ya mumewe na kupata majibu yake. Mwanasoshalaiti huyo alipohojiwa na Nairobi News, aliweka wazi kwamba anaendelea vizuri na watoto wao pia walikuwa sawa.

"Niko sawa, na mtoto wangu anaendelea vizuri. Sifanyi mahojiano yoyote kwa sasa tafadhali,” alisema kabla ya kutoweka.

Upekuzi kwenye akaunti ya Instagram ya mwanasoshalaiti huyo umebainisha kuwa bado angali anamfuatilia mwimbaji huyo na picha zao bado zilikuwepo kufikia siku ya Jumanne, Aprili 18 mwendo wa saa saba adhuhuri.

Siku ya Jumanne, Brown Mauzo alichapisha video ya binti yao, Asia Brown na kuambatanisha na ombi maalum kwake.

"Malkia wangu mdogi @princess_asiabrown. Mwenyezi Mungu akulinde," aliandika chini ya video ya mtoto huyo wa mwaka mmoja.

Haya yanajiri huku wanandoa hao wakiwa wanatarajia mtoto wao wa pili pamoja. Wawili hao ambao wamekuwa wakichumbiana kwa zaidi ya miaka miwili walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza mwaka wa 2021.

Mwishoni mwa mwaka jana, Vera alifichua atafunga pingu za maisha na mzazi huyo mwenzake mwaka wa 2023 au 2024.

Mara kadhaa amefafanua kwamba wapo kwenye ndoa rasmi ila bado hawajafanya harusi ya umma.

"Umewahi kufikiria kufanya harusi nyeupe?" shabiki alimuuliza mwezi Novemba mwaka jana.

Mama huyo wa mtoto mmoja alijibu: "Ndiyo. Tunafikiria mwisho wa 2023 au mwanzoni mwa 2024. Mimi ni mpenda ukamilifu kwa hivyo ningependa kuchukua muda kupanga kila undani t ukamilifu,".

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba atafikiria kupanua familia yake tena baada ya miaka sita.

Vera Sidika hata hivyo alifichua kuwa mume wake, mwimbaji Brown Mauzo anataka sana wapate watoto kumi pamoja.

"Mume wangu anataka watoto kumi. Kwa upande wangu, sio wakati wowote hivi karibuni. Labda nitaongezea mwingine mmoja baadaye kabisa baada ya miaka sita," alisema.

Wawili hao wamekuwa wakichumbiana tangu mwaka wa 2020 na hivi karibuni wanatarajia mtoto wa kiume pamoja.