Amber Ray azungumzia yeye na Rapudo kufukuzwa kwa nyumba yao, afichua maelezo ya kuachana kwao

Amber Ray aliweka wazi kuwa yeye na Kennedy Rapudo walitengana kwa sababu ya tofauti zao.

Muhtasari

• Amber Ray amepuuzilia mbali madai kwamba yeye na Rapudo walitengana kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kulipa kodi ya nyumba.

•Amber Ray aliweka wazi kuwa hawakufukuzwa kutoka kwa nyumba yao na pia alifichua kuwa hawakuwa na deni la kodi walikuwa wakiondoka.

KENNEDY RAPUDO WAKIWA NA AMBER RAY.
KENNEDY RAPUDO WAKIWA NA AMBER RAY.
Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mwanasosholaiti mashuhuri wa Kenya Faith Makau almaarufu Amber Ray amepuuzilia mbali madai kwamba yeye na mzazi mwenzake Kennedy Rapudo walitengana kwa sababu hawakuwa na uwezo tena wa kulipa kodi ya nyumba yao ya kupanga yenye vyumba vya kulala vitano.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne, mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa yeye na Rapudo walitengana kwa sababu ya tofauti zao.

Alidokeza kuwa kulipa kodi ya jumba lao la kukodi haikuwa shida kamwe na akaeleza kuwa wote wawili walihama kwa kuwa hawakuwa wanaishi pamoja kama familia kubwa.

“Mimi na Ken tulitengana kwa sababu ya tofauti zetu, si kwa sababu hatukuweza kudumisha nyumba yetu. Na kwa hakika haikuwa kutafuta kiki. Sipendi kutafuta kiki, haswa sio kwa mambo ya kibinafsi sana. Licha ya watu wengi kufahamu kilichotokea, bado ni suala la kibinafsi na ni moja ambalo linatatuliwa,” Amber Ray alisema.

Aliongeza, "Kodi haikuwa shida kamwe. Nilihama katikati ya mwezi, na Ken alihama muda mfupi baadaye. Haingekuwa na maana kwake kukaa katika nyumba ya vyumba 5 vya kulala akiwa peke yake."

Mrembo huyo aliweka wazi kuwa hawakufukuzwa kutoka kwa nyumba yao na pia alifichua kuwa hawakuwa na deni la kodi walikuwa wakiondoka.

Aidha, alifichua kuwa kodi ya nyumba zao mpya zikijumuishwa ni kubwa kuliko kiasi walichokuwa wakilipa katika nyumba waliyokuwa wakiishi pamoja.

"Sijaribu kujitetea, lakini singependa kuharibu sifa yangu kwa habari za uwongo mtandaoni. Na kwa heshima zote, watu wanapaswa kuzingatia mambo yao wenyewe, " alisema

Mama huyo wa watoto wawili alichukua fursa hiyo kuwaomba watu kuwapa sapoti wanaopitia changamoto kama yeye badala ya kuwashambulia mtandaoni.

Katika siku kadhaa za hivi majuzi, kumekuwa na tetesi kuwa Amber Ray na mzazi mwenzake Kennedy Rapudo walitengana baada ya kushindwa kulipia nyumba yao.