Babake Diamond Platnumz amwagiza aoe, abadili tabia zake

Mzee Abdul alidokeza kuwa mwimbaji huyo amezingirwa na watu wasiompa ushauri sahihi.

Muhtasari

•Mzee Abdul alikosoa baadhi ya masuala katika maisha ya mwanawe ikiwa ni pamoja na hatua yake ya hivi majuzi ya kutobolewa pua.

•Mzee Abdul alikiri kuwa muda mrefu umepita tangu alipomuona mwanawe huyo kwa mara ya mwisho.

Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Image: HISANI

Mzee Abdul Juma Isack amemshauri anayeaminika kuwa mwanawe, Diamond Platnumz kuhusu masuala mbalimbali ya kimaisha.

Katika mahojiano na Mbengo TV, Mzee Abdul alidokeza kuwa mwimbaji huyo amezingirwa na watu wasiompa ushauri sahihi.

Alikosoa baadhi ya masuala katika maisha ya mwanawe ikiwa ni pamoja na hatua yake ya hivi majuzi ya kutobolewa pua.

"Aachane na mambo ya kuiga, aende na maadili ya kitanzania. Kama kuna uwezekano aoe. Pia afuatilie yale ambayo anaweza kuyafanya, asifanye vitu ambavyo vitawashangaza wananchi ama wapenzi wake ," alisema.

Mzee Abdul alibainisha kuwa staa huyo wa Bongo ana uwezo na uhuru wa kufanya jambo lolote atakalo na maisha yake, lakini akamsihi azingatie maadili ya jamii yake ya Kitanzania na ya dini yake ya Kiislamu.

"Kama kuna uwezekano abadilishe. Kabla afanye kitu aombe ushauri wa bure. Katoboa pua ndio lakini hayo sio maadili ya Kitanzania, hayo ni maadili ya kiajabu ajabu. Wako wabaofanya lakini sio watu wa kwao," alisema.

Alisema ikiwa mapenzi yake na Mama Dangote ni  mwanawe kutobolewa pua basi wangechukua hatua hiyo kitambo.

Aliwasihi watu wa karibu na Diamond kumpa ushauri kuhusu maadili mema ya maisha ili asije akapotoka.

"Naomba wamsawazishe. Wasimuogope kwa sababu ana uwezo. Kapewa vitu na mwenyezi Mungu, basi avitumie vizui"

Mzee Abdul alikiri kuwa muda mrefu umepita tangu alipomuona mwanawe huyo kwa mara ya mwisho. Hata hivyo alieleza matumaini yake kuwa siku moja bosi huyo wa WCB atachukua hatua ya kumtembelea.

"Huenda ana pilkapilka nyingi za kikazi. Labda anakosa kutulia akitafuta maisha.  Ipo siku atakuja kunipa salamu," alisema.

Miezi michache iliyopita Diamond aliweka wazi kwamba hana nia ya kuoa hivi karibuni akidai kuwa hatua hiyo ingezorotesha taaluma yake. Hata hivyo imekuwa ikidaiwa kuwa yupo kwenye mahusiano ambayo bado hajafichua.

Bosi huyo wa WCB amekuwa akidaiwa kuchumbiana na msanii wake Zuchu, madai ambayo wote wawili wamekuwa wakikana.