“Bado anaitwa hivyo!” Mulamwah ajibu kwa kejeli baada ya kuulizwa kuhusu binti yake

Mulamwah alijaribu kukwepa kujibu swali hilo kabla ya kutania kuhusu kutokuwa na uhakika anaitwaje siku hizi.

Muhtasari

•Katika mahojiano na waandishi wa habari, Mulamwah alitakiwa kueleza jinsi msichana huyo wa miaka miwili anavyoendelea.

•Jioni hiyo hiyo, mchekeshaji huyo alithibitisha kuwa ana mtoto mmoja ambaye anajulikana hadharani.

katika picha ya maktaba.
Mulamwah na binti yake katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji maarufu wa Kenya David Oyando almaarufu Kendrick Mulamwah alitoa jibu la kejeli baada ya kuhojiwa kuhusu binti yake, Keilah Oyando.

Katika mahojiano na mwanahabari wa mtandaoni Vincent Mboya Jumatano jioni, alitakiwa kuzungumzia jinsi msichana huyo wa miaka miwili anavyoendelea.

“Keilah anaaendeleaje?” Mboya alimuuliza Mulamwah.

Mwanzoni, msanii huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana kujaribu kukwepa kujibu swali hilo kabla ya kutania kuhusu kutokuwa na uhakika anaitwaje siku hizi.

“Bado anaitwa hivyo?” Mulamwah alisema kwa utani huku akiwatoka waandishi wa habari.

Jioni hiyo hiyo, hata hivyo alimthibitishia mwanahabari wa Mpasho, Kalondu Musyimi kuwa ana mtoto mmoja ambaye anajulikana hadharani.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mchekeshaji huyo na aliyekuwa mpenzi wake, Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie kutupiana lawama hadharani kuhusu utunzaji wa binti yao mrembo.

Takriban wiki mbili zilizopita, Mulamwah alileza nia yake ya kusaidia katika malezi ya mtoto wake wa pekee na Carrol Sonnie.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, baba huyo wa mtoto mmoja hata hivyo alidai kwamba haijakuwa rahisi kwake kuhusika katika maisha ya bintiye.

Alidai kuwa kila anapotuma pesa au zawadi za kumtunza binti huyo wake wa miaka miwili, hurejeshwa kwake.

"Ninajaribu kusaidia lakini sio rahisi. Unatuma pesa zinareversiwa. Hata birthday nimetuma zawadi ikarudishwa. Hivyo inakuwa ngumu sana,” Mulamwah alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa anasaidia katika malezi ya bintiye.

Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alibainisha kuwa haelewi tatizo liko wapi kati yake na mpenziwe huyo wa zamani.

Muda mfupi baada ya Mulamwah kuibua madai hayo, Sonnie alionekana kuthibitisha kuwa kweli huwa anarudishia pesa na usaidizi mwingine ambao mpenzi huyo wake wa zamani hutuma  kwa ajili ya malezi ya binti yao.

Muigizaji huyo alitoa taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiashiria sababu ya kutokubali usaidizi wa Mulamwah ambapo alizungumza kuhusu kutokubali ofa zinazokuja bila heshima.

"Habari za asubuhi. Kikumbusho tu cha haraka. "Haijalishi umefirisika kiasi gani, USIKUBALI kupokea matoleo yanayokuja na UKOSEFU WA HESHIMA," Sonnie aliandika.

Chapisho la muigizaji huyo lilionekana kama jibu lisilo la moja kwa moja kwa madai yaliyotolewa na mpenziwe wa zamani alipokuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram.