Baha na mpenziwe wazungumza kuhusu safari ya ujauzito wa mtoto wao wa kwanza

Muhtasari

•Georgina alifichua kwamba alikuja kugundua kuhusu ujauzito wake mwishoni mwa mwezi Oktoba, mwaka jana.

•Baha kwa upande wake alifichua kuwa haijakuwa rahisi kushughulika na kipenzi chake katika kipindi hiki cha ujauzito.

Image: INSTAGRAM// KAMAU MBAYA

Hatimaye mwigizaji Kamau Mbaya almaarufu Baha kutokana na kipindi 'Machachari' na mpenzi wake Georgina Njenga wamefichua kwamba wanatarajia mtoto wao wa kwanza.

Wapenzi hao wawili walitangaza kuhusu ujauzito wao siku ya Jumatatu kupitia kurasa  zao za mitandao ya kijamii.

Kupitia kanda ya video ambayo walipakia YouTube, wawili hao waliweka wazi kuwa wapo tayari kwa hatua ya kuwa wazazi.

Georgina alifichua kwamba alikuja kugundua kuhusu ujauzito wake mwishoni mwa mwezi Oktoba, mwaka jana.

"Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito wangu imekuwa laini. Isipokuwa tumbo kunenepa na kukumbwa na kiungulia cha moyo, hakuna dalili zingine," Alisema.

Baha kwa upande wake alifichua kuwa haijakuwa rahisi kushughulika na kipenzi chake katika kipindi hiki cha ujauzito.

Alisema mpenziwe amekuwa akikumbana na mabadiliko ya hisia huku akimtaja kama "mayai moto inayokuchoma"  katika kipindi cha ujauzito wake.

"Ananitolea tu mataa, kila wakati mabadiliko ya hisia. Kila kitu katika safari hii ya ujauzito anasema 'ni mtoto'," Alisema.

Baha alisema angependa wapate mtoto wa kiume ilhali mpenziwe kwa upande wake angetaka mtoto wa kike.