Daddy Owen ajibu madai ya mkewe kumtema na kuendea mwanaume tajiri

“Ndoa yangu kuisha iliisha. Haikuisha vizuri. Kwa kweli, kuna stori nyingi zilitoka. Zingine kweli, zingine hazikuwa kweli," Daddy Owen alisimulia.

Muhtasari

•Daddy Owen alifichua kwamba alikuwa kwenye ndoa na mzazi huyo mwenzake huyo kwa takriban miaka mitano kabla ya kuvunjika kwa njia mbaya.

•Daddy Owen alidokeza kuwa licha ya shinikizo, hakuwa tayari kumsema vibaya mzazi huyo mwenzake kwa ajili ya watoto wao.

Daddy Owen na aliyekuwa mkewe, Faridah Wambui
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amezungumza kwa undani kuhusu talaka yake na aliyekuwa mke wake Faridah Wambui iliyotokea mwaka wa 2020.

Katika mahojiano na Mwafrika kwenye kipindi cha Iko Nini podcast, baba huyo wa watoto wawili alifichua kwamba alikuwa kwenye ndoa na mzazi huyo mwenzake huyo kwa takriban miaka mitano kabla ya kuvunjika kwa njia mbaya.

Daddy Owen alibainisha kuwa hadithi nyingi zilitokea baada ya talaka, ambazo baadhi anasema zilikuwa za kweli ilhali zingine zilikuwa habari za uwongo.

“Ndoa yangu kuisha iliisha. Haikuisha vizuri. Kwa kweli, kuna stori nyingi zilitoka. Zingine kweli, zingine hazikuwa kweli lakini ndoa yangu iliisha. Ilichukua muda kujua nini cha kufanya baadae. Haikusha poa, kwa kweli mlisikia stori mob,” Daddy Owen alisema.

Ingawa hakuzungumza wazi kuhusu kilichovunja ndoa yake, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 41 alitwikwa jukumu la kujibu madai kwamba mke wake wa zamani alinyakuliwa na mfanyibiashara mbwenyenye.

Huku akijibu swali hilo, Daddy Owen alimfahamisha Mwafrika kuwa hana uhuru wa kuzungumzia tuhuma hizo kwani zinaweza kusababisha masuala ya mahakama.

“Kuna mambo mengine ni noma sana kuongea kwa sababu hii stori ilienda mpaka kortini. Siwezi taka ukuje userviwe hapa juu ya kitu huwezi kuelewa,” alisema.

Mwanamuziki huyo wa injili pia alizungumzia jinsi mashabiki wake, vyombo vya habari na wanablogu walivyomsukuma sana kuchafua jina la Bi Faridah, jambo ambalo hakuwa tayari kufanya.

“Mitandao iliongea mambo mengi. Tofauti ilikuwa, singeweka kutoka huko nje nianze kuweka mambo wazi na kusema hii ni kweli, hii ni uongo. Jambo moja nililogundua wakati huo, mtandao ulikuwa ukinisukuma sana. Wanablogu, watu wa vyombo vya habari na hata mashabiki walikuwa wakinisukuma kuchafua jina la mke wangu wa zamani,” alisema.

Hata hivyo alidokeza kuwa licha ya shinikizo hilo, hakuwa tayari kumsema vibaya mzazi huyo mwenzake kwa ajili ya watoto wao.

“Mimi sikudhani ni ya maana. Licha ya yaliyomo, siwezi enda mahali nianze kuweka jina lake, nitasaidika na nini. Siwezi. Sio mimi na ni kitu siwezi kufanya,” alisema.

Daddy Owen na Bi Faridah Wambui walikutana mwaka wa 2012, wakafunga ndoa mwaka wa 2016 kabla ya kuachana 2020.