Dhana potovu zinazohusishwa na vijana waliofanikiwa nchini Kenya

Uhalifu, ibada za shetani na Wash Wash ni baadhi ya mambo ambayo vijana waliofanikiwa wamehusishwa nayo

Muhtasari

•Willy Paul alihusishwa na ibada za shetani baada ya kutangaza gari lake mpya aina ya Mercedes Benz.

•Vijana Wakenya wamehusishwa na biashara haramu ya madawa baada ya kuonekana wakijigamba na pesa nyingi, wakiendesha magari makubwa na kuwa vipenzi vya wanawake.

Thee Pluto, KRG The Don, Willy Paul
Image: HISANI

Hivi majuzi mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Willy Paul alikuwa mwathirika wa ukosoaji mkubwa mitandaoni baada ya kufichua gari lake jipya.

Jumamosi, staa huyo alizua gumzo kubwa katika mtandao wa Instagram baada ya kuchapisha video iliyoonyesha gari mpya aina ya Mercedes Benz lenye nambari ya usajili 666 ambayo aghalabu huhusishwa na ibada ya shetani.

“Mungu alitenda tena!!! Atukuzwe Mungu aliye juu.. asante Baba yangu kwa zawadi nyingine nzuri. Niliamua kujipa zawadi kwa kazi nzuri ambayo nimekuwa nikifanya, kwa MAUDHUI SAFI ambayo nimekuwa nikitoa," alisema chini ya video hiyo.

Licha ya kumshukuru Mungu kwa mafanikio hayo, baadhi ya wanamitandao walimhusisha msanii huyo kijana na ibada za shetani.

Kuabudu Shetani ni jambo moja tu ambalo Wakenya na Waafrika kwa ujumla mara nyingi huwahusisha vijana waliofaulu nalo. Baadhi ya madai huenda yakawa ya kweli ilhali vijana wengine waliofaulu ni wahasiriwa wa mashtaka ya uwongo tu.

Dhana zingine zinazohusiana na mafanikio miongoni mwa vijana ni pamoja na:-

ii) Biashara ya madawa ya kulevya:-

Sio tukio moja tu ambapo vijana Wakenya wamehusishwa na biashara haramu ya madawa baada ya kuonekana wakijigamba na pesa nyingi, wakiendesha magari makubwa na kuwa vipenzi vya wanawake.

Ingawa biashara hiyo si ngeni miongoni mwa vijana, si lazima iwe kwamba wale waliovuka daraja la umaskini wanaiendeleza.

iii) Wash Wash

Wash Wash ni jina maarufu la biashara haramu na hatari ya utakatishaji pesa hapa nchini Kenya. Biashara hiyo ilipata umaarufu mkubwa mwaka jana kufuatia ufichuzi wa vyombo mbalimbali vya habari.

Baada ya ufichuzi huo, vijana wengi hasa wasanii wenye uwezo mkubwa wa kifedha wamehusishwa na biashara hiyo.

Mwanavlogu Thee Pluto, mwimbaji KRG The Don, Mbunge Jalang'o na Mtangazaji Betty Kyallo ni miongoni mwa wasanii ambao wamewahi kujitokeza kujitenga na madai ya Wash Wash baada ya kuhusishwa na biashara hiyo.

iv)  Uhalifu

Vijana wengi waliofanikiwa wamehusishwa na uhalifu wa aina mbalimbali kama vile ujambazi,  utekaji nyara n.k. baada ya kujizolea utajiri ghafla.

Uhalifu ni mtindo wa kawaida miongoni mwa vijana hasa katika maeneo ya mijini lakini hata si lazima mtu awe amejiingiza katika uovu huo ili kufanikiwa.

v) Ulaghai

Vijana kadhaa waliofaulu nchini Kenya hapo awali wamewahi kushutumiwa kujipatia mali zao kwa kulaghai watu. Baadhi wamedaiwa kulaghai watu kupitia biashara za mitandaoni kama vile bitcoins, cryptocurrency n.k.

Vijana waliopatikana wameuawa katika hali tatanishi mnamo mwezi Juni  Frank Obegi, Fred Obare, Moses Nyachae na Elijah Omeka walidaiwa kujihusisha na ulagahai wa mitandaoni, jambo lililopelekea mauti yao.

vi)  Kuuza picha na video za uchi

Baadhi ya vijana wamedaiwa kujihusisha na biashara za picha za ngono katika juhudi za kuvuka daraja la umaskini.

Ingawa madai mengine yamedhibitishwa kuwa ya kweli, baadhi ya waliokabiliwa na shutuma hizo hawana hatia na ni wahasiriwa tu wa dhana potovu.