Esther Musila azungumzia alivyotakiwa kifo na kudaiwa kumwambukiza Guardian Angel Ukimwi

Musila alitaka kuchukua hatua za kisheria alipodaiwa kumuambukiza mumewe virusi vya Ukimwi.

Muhtasari

•Musila amekuwa akishambuliwa mtandaoni kwa muda mrefu haswa baada ya mahusiano yake na Guardian Angel kufichuka.

•Alisema kufikia sasa tayari ameblock akauti takriban 5,000 za wanamitandao ambao waliwahi kumshambulia.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Image: INSTAGRAM//GUARDIAN ANGEL

Bi Esther Musila, mke wa mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, sio mgeni kwa unyanyasaji wa mitandaoni.

Musila amesema amekuwa akishambuliwa mtandaoni kwa muda mrefu haswa baada ya mahusiano yake na Guardian Angel kuwa hadharani.

"Awali akaunti zangu zote zilikuwa zimefungwa kwa watu wa karibu tu hadi wakati ambapo nilifunuliwa kwa ulimwengu wa nje nilipokutana na mume wangu. Nilifunuliwa kwa ulimwengu huu ambao sikuwa na uzoefu wowote kuuhusu. Ilikuwa ngumu, kila mtu alikuwa kwenye kesi yangu kwa sababu ya hali yangu," Musila alisema katika mahojiano na Digital Dada Podcast.

Mama huyo wa watoto watatu alifichua kwamba siku za mwanzo angeathirika vibaya hadi kufikia hatua ya kulia kila aliposhambuliwa mitandaoni.

Alifichua kuwa shambulizi lililomuathiri zaidi ni ambalo mtumizi mmoja wa mitandao alimtakia kifo kabla ya mumewe.

"Mtu alinitumia meseji, sikumjua, akasema 'Utakufa kabla ya Guardian, nakutakia kifo' . Niliangalia meseji hiyo, ilikuwa imetumwa saa kumi na moja na dakika 27 asubuhi. Nilitoka kwa kitanda nikaenda sebuleni nikatafakari huyo mtu hakulala akifikiria kunihusu kwa sababu gani. Ilifanya nifikirie kwani watu wanaweza kuwa wakatili kiasi gani. Nilijiuliza nimefanya nini?," Alisema.

Musila alimjibu mshambulizi huyo wake na kumshauri asiwahi kutakia mwingine kifo kisha akablock akaunti yake.

Alisema kufikia sasa tayari ameblock akauti takriban 5,000 za wanamitandao ambao waliwahi kumshambulia.

"Sitaki mambo hasi katika nafasi yangu. Chapisho zangu huwa kuhusu mambo mazuri tu. Licha ya masuala na shida zote tulizo nazo, naamini katika kuwa na hali nzuri. Hiyo ndiyo najihubiria," Alisema

Mke huyo wa Guardian Angel pia alifichua kuwa kwa kawaida huwa hasomi blogu zinazochapisha habari za uwongo.

Hata hivyo wakati mmoja aliwahi kutaka kuchukua hatua za kisheria baada ya kudaiwa kumuambukiza mumewe virusi vya Ukimwi.

"Waliandika  kuwa niko na virusi vya Ukimwi na nimeambukiza mume wangu," Alisema.

Musila alisema kwa sasa haathiriwi na mashambulizi ya mitandaoni wala habari za uwongo kwani huwa anapuuzilia yote.