"Familia muhimu!" Lilian Nganga asikitika kuhusu marafiki bandia kufuatia mazishi ya Chiloba

Nganga amewabainishia watu kwamba familia ndio muhimu zaidi.

Muhtasari

• Lilian Nganga amewashtumu wengi wao ambao walimuomboleza Chiloba mitandaoni tu na kukosa kuhudhuria mazishi yake kwa kuwa marafiki bandia na wa kujifanya tu.

•Kulingana na Ntalami, baadhi yao walijitokeza na kutoa heshima zao kwa njia ambazo watu hawawezi kuzifahamu.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Suala la mduara wa marafiki wa mwanaharakati wa haki za LGBTQ Edwin Chiloba limeendelea kuwa kubwa mada miongoni mwa Wakenya wiki kadhaa baada ya kuuawa.

Chiloba alizikwa nyumbani kwao Sergoit, kaunti ya Elgeyo Marakwet siku ya Jumanne baada ya kupatikana ameuawa mapema mwezi huu. Rafiki yake Jackton Odhiambo ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji yake na kwa sasa anazuiliwa pamoja na wengine wanne.

Kufuatia mauaji ya mwanaharakati huyo mapema mwezi huu, Wakenya wengi walijitokeza kumuomboleza na kulaani mauaji yake huku wengine wakifichua matukio yao ya nyuma naye na uhusiano wa karibu naye.

Mke wa mwimbaji  wa nyimbo za kufoka Juliani, Lilian Nganga hata hivyo amewashtumu wengi wao ambao walimuomboleza Chiloba mitandaoni tu na kukosa kuhudhuria mazishi yake kwa kuwa marafiki bandia na wa kujifanya tu

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nganga sasa amewatahadharisha watu kuhusu marafiki wa kujifanya huku akiwabainishia kwamba familia ndio muhimu zaidi.

"Kwamba watu wengi waliochapisha jinsi walivyojua Chiloba hawakuhudhuria mazishi yake inaonyesha jinsi urafiki wa juu juu ulivyo na kwamba familia ndiyo jambo muhimu," Nganga alisema kwenye Instastori.

Mwili wa marehemu Chiloba ulizikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Sergoit, Keiyo Kaskazini, Elgeyo Marakwet mnamo Jumanne, Januari 17.

Mamia ya waombolezaji, wengi wakiwa wanafamilia, majirani na watu wa karibu walitoa heshima za mwisho kwake katika hafla hiyo iliyojaa hisia.

Baada ya maziko ya marehemu, mmoja wa marafiki zake wa karibu Michelle Ntalami alieleza kwa nini hakuhudhuria. Kulingana na Michelle, baadhi yao walijitokeza na kutoa heshima zao kwa njia ambazo watu hawawezi kuzifahamu.

"Wale ambao hawakuweza au hawangeweza kuenda sio eti wanampenda kidogo! Wewe ni mmoja wa wale wanamitandao wanaosubiri tu kuona ni nani waliohudhuria na ambao hawakuhudhuria ili kufanya waonekane wabaya," Michelle alimjibu mtumizi mmoja wa Instagram ambaye alihoji kwa nini hakuwepo.

Michelle na Chiloba walikuwa marafiki na hata alifichua kuwa marehemu alimpa maua siku ya wapendanao mwaka jana.