Georgina Njenga tayari kujaribu ndoa tena baada ya ile ya kwanza na Baha kugonga mwamba

Georgina alidokeza kwamba ana mpango wa kujaribu ndoa tena lakini hana uhakika kuhusu kupata watoto zaidi.

Muhtasari

•Georgina alitakiwa kujibu iwapo anawaza kujitosa tena kwenye ndoa baada ya uhusiano wake na Baha kugonga mwamba mapema mwaka huu.

•Alipoulizwa kuhusu anachopendelea kati ya kuolewa na kuwa bila mchumba, alibainisha kuwa chaguzi zote mbili zina madhara yake.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Mtayarishaji  wa Maudhui Georgina Njeri Njenga aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram siku ya Alhamisi jioni ambapo alifunguka kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake, mahusiano na mambo mengine.

Katika mojawapo ya maswali aliyoulizwa, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alitakiwa kujibu iwapo anawaza kujitosa tena kwenye ndoa baada ya uhusiano wake na muigizaji Tyler Kamau Mbaya almaarufu Baha wa Machachari kugonga mwamba mapema mwaka huu.

Pia aliulizwa kama ana nia ya kupata mtoto mwingine katika siku zijazo.

“Utawahi kuolewa tena?? Au kuzaa tena?,” shabiki mmoja aliuliza.

Katika majibu yake, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba ana mpango wa kujaribu ndoa tena katika siku zijazo lakini hana uhakika kuhusu kupata watoto zaidi.

"Kuolewa, ndio .. kuhusu watoto, hapana. Lakini huwezi kujua maishani,” Georgina alijibu.

Wakati alipoulizwa kuhusu anachopendelea kati ya kuolewa na kuwa bila mchumba, alibainisha kuwa chaguzi zote mbili zina madhara yake.

"Zote ziko na madhara.. chagua mapambano yako kwa busara," alisema.

Georgina alithibitisha kuachana na mzazi mwenzake Tyler Mbaya takriban miezi minne iliyopita ambapo pia alifichua kuwa tayari yuko kwenye uhusiano mwingine.

Alifunguka kuhusu mwisho wa uhusiano wake na Tyler alipokuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi kingine cha maswali na majibu kwenye Instagram.

"Wengi wenu mnauliza swali hili. Hii ni mara ya mwisho nitajibu. Tuliachana na niko kwenye uhusiano mpya na mwanamume wangu mpya,” Georgina alisema.

Katika mahojiano na Mungai Eve mnamo Agosti, Georgina alieleza kuwa uhusiano wao uliisha kwa amani baada ya majaribio kadhaa ya kujaribu kufanya mambo yawe sawa.

Walakini, mtayarishaji huyo wa maudhui aliweka wazi kuwa licha ya kwenda njia tofauti, Baha bado anahusika katika maisha ya mtoto wao.

“Hakukuwa na sababu maalum; haikuwa inafanya kazi tu. Siwezi kubainisha jambo moja. Siwezi kusema alifanya hivi au vile au nilifanya vile. Masuala yalilundikwa… na inafikia wakati unagundua kuwa hii haifanyi kazi. Kwanza kabisa, hakuna hata mmoja wetu aliyeamua kwamba amemuacha mwingine lakini makubaliano ya pande zote juu ya hili hayafanyiki. Kwa hiyo hakuna aliyemuacha mwingine, tulijadiliana na kukubaliana kwamba hatuwezi kuendelea,” Georgina alisema kwa sehemu.

Aliendelea; "Unajua wakati umejaribu kuzungumza kwa muda mrefu na inafikia hatua ukaamua hatuwezi tena,".

Alipoulizwa iwapo walijaribu kuwashirikisha wazazi wao katika kuokoa uhusiano huo, Georgina alijibu; "Ndiyo tulifanya hivyo.”