"Hakikisha umejijenga kwanza kabla ya kujitosa kwenye ndoa " Carol Muthoni awashauri wanadada

"Tafuta pesa ujijenge kwanza. Mengine yatajileta," Alisema.

Muhtasari

•Muthoni aliwashauri wanawake kuhakikisha kuwa wako sawa kifedha, kiakili na kihisia kabla ya kujitosa kwenye ndoa.

•Muthoni pia alifichua kuwa wanaume wengi wamekuwa wakimmezea mate. Hata hivyo amewasihi watulie kidogo kwanza. 

Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie amewashauri wanadada kutokubali shinikizo la jamii kuhusu umri mwafaka wa kuolewa.

Akizungumza kwenye ukurasa wake wa Instagram, Muthoni alisema kwamba umri sio jambo muhimu zaidi kuzingatia katika mpango wa ndoa.

Mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji Mulamwah aliwashauri wanawake kuhakikisha kuwa wako sawa kifedha, kiakili na kihisia kabla ya kuzamia kwenye ndoa.

"Olewa ukiwa tayari. Hakikisha uko katika nafasi ambayo unaweza kujisimamia, usitegemee mpenzi wako. Wanawake, kabla ya kuingia kwenye ndoa tafadhali hakikisha umejijenga kwanza. Kuwa sawa kiakili, kifedha na kihisia," Muthoni alisema.

Mama huyo wa binti mmoja aliwahimiza wanawake kukimbiza ndoto zao kwanza huku akiwahakikishia kwamba mengine yatajileta baadae.

"Tafuta pesa ujijenge kwanza. Mengine yatajileta," Alisema.

Muthoni pia alifichua kuwa wanaume wengi wamekuwa wakimmezea mate. Hata hivyo amewasihi watulie kidogo kwanza.