Hamisa Mobetto hatimaye amtambulisha mwanaume anayemmezea mate

Mapema mwezi huu Mobetto alidokeza kuwa amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba.

Muhtasari

•Mobetto alichapisha video ya mkusanyiko wa picha kadhaa za Jordan na kumtambulisha kama mwanamume ambaye angetaka kuolewa naye.

•Michael B. Jordan, 35, ni muigizaji wa Marekani, mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Hamisa Mobetto

Mwanamitindo na mwimbaji wa Bongo Hamisa Mobetto amekiri mapenzi yake makubwa kwa muigizaji wa Marekani Michael B. Jordan.

Kwenye akaunti yake ya tiktok, mama huyo wa watoto wawili alichapisha video ya mkusanyiko wa picha kadhaa za Jordan na kumtambulisha kama mwanamume ambaye angetaka kuolewa naye.

"Ona mvulana ninayetaka kuolewa naye 😩❤️💍👉🏼" aliandika chini ya video hiyo iliyoanza na picha yake.

Michael B. Jordan, 35, ni muigizaji wa Marekani, mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu. Anajulikana kwa uhusika wake katika filamu maarufu kama The Wire (2002) Fruitvale Station (2013), Creed (2015) na Black Panther (2018, 2022).

Mwaka wa 2020, Jordan alitajwa kuwa mmoja wa watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni na jarida la Time na pia kama mwanaume mzuri zaidi aliye hai.

Muigizaji huyo alijitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamitindo wa Marekani Lori Harvey mnamo Novemba 2020 . Mwezi Juni 2022 ilitangazwa kuwa wasanii hao wawili walikuwa wametengana.

Mapema mwezi huu Hamisa Mobetto alitangaza wazi kuwa amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba.

Katika video aliyochapisha mitandaoni, mzazi mwenza huyo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alikiri mapenzi yake mazito kwa mpenzi wake mpya na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

"Hatimaye nimepata mtu. Nimepata mwanaume ambaye nahisi ni yeye nataka. Nahisi kama kwamba huyu ndiye mtu ningependa kushiriki maisha yangu yote naye," alisema kwa kujivunia na msisimko mkubwa.

Mobetto aligamba kwamba hatimaye amefanikiwa kupata mwanamume anayezungumza lugha ya mapenzi sawa na yeye.

"Kila kitu ni rahisi sana, kila kitu ni sawa" alisema.

Aidha alisema kuwa anatamani sana kuvishwa pete na mpenzi wake mpya na kuchukua majukumu ya mke.

"Nataka kuolewa naye. Nataka kuolewa na mtu wangu. Nataka kumpikia, nimuandalie nguo ili aende kazini. Je, hii ni ndoto? niamke? Ikiwa ni ndoto mtu tafadhali anichune niamke," alisema Mobetto.

Ingawa hakumtambulisha mpenziwe, Mobetto alimsifia sana na kusema kuwa yeye ndiye mume kamili kwake.

"Ni kijana mzima. Ni mwananaume mwenye tabia njema. Ananukia vizuri. Anaongea vizuri,"alisema kwa madaha.

Mobetto alisema kuwa anasubiri kwa hamu jinsi mambo yatakavyokuwa wakati atakapokuwa kwenye ndoa naye.