Harmonize afichua sababu kuu ya ugomvi wake na Diamond

"Ni pressure ya kuhofia nampita. Akiskia nakohoa karoho kanampita," Harmonize alisema.

Muhtasari

•Harmonize ameweka wazi kuwa hakuwahi kutaka kugombana na Diamond ila bosi huyo wake wa zamani alianza kumuoenea kijicho.

•Harmonize alibainisha kuwa hayuko kwenye ushindani na mtu yeyote licha ya mara nyingi kushindanishwa na Diamond.

katika picha ya maktaba.
Harmonize na Diamond katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worlwide Harmonize ameendelea kuachia nyimbo zilizo  kwenye albamu yake mpya 'Made For Us'.

Albamu hiyo ya tatu ya Harmonize ina jumla ya nyimbo 14 na karibu kila kibao pale kina hadithi nyuma yake au mlengwa.

Wimbo ambao umekuwa ukifanya vizuri ni wa pili 'My Way' ambao ametumia kutupa vijembe kwa watu kadhaa maishani mwake. Bosi wake wa zamani katika WCB Diamond hajasazwa nyuma katika wimbo huo.

Katika sehemu ya wimbo huo, Konde Boy  ameweka wazi kuwa hakuwahi kutaka kugombana na Diamond ila bosi huyo wake wa zamani alianza kumuoenea kijicho. Alibainisha kuwa hakuwahi kuwa na shida na watu waliojaribu kumzuia hapo awali

"Hata huyo ndugu yenu mi sikuvitaka vita. Mbona sikugombana na Madam Rita? Ni pressure ya kuhofia nampita. Akiskia nakohoa karoho kanampita," aliimba.

Aidha, staa huyo wa Bongo alibainisha kuwa hayuko kwenye ushindani na mtu yeyote licha ya mara nyingi kushindanishwa na Diamond.

"Siishi kwa matakwa mtu, siwezi mridhisha kila mtu. Eti nisifanye kitu kumuogopa. Huu muziki ni kipaji sishindani na mtu," alisema.

Pia alibainisha kuwa amejikita katika kujaribu bahati yake maishani na anawajali tu watu wake wa karibu.

Siku chache zilizopita Diamond alionekana kuandaa jukwaa lingine la vita na Harmonize baada ya kuweka tarehe ya kuachia EP ya msanii wake Mbosso siku moja tu kabla ya uzinduzi wa albamu ya Harmonize.

Wikendi iliyopita Harmonize alitangaza kwamba angezindua Albamu yake mpya 'Made for Us' mnamo Oktoba 28. Muda mfupi baadae, lebo ya Diamond ya WCB pia ilifichua mipango ya kuzindua EP ya Mbosso.

Harmonize alivunja uhusiano wake na Diamond na kuondoka WCB Wasafi mwishoni mwa 2019. Tangu wakati huo amefanya miradi kadhaa akiwa peke yake na hata kuanzisha lebo yake ya muziki, Konde Music Worlwide