Harmonize apumzika kumtongoza Kajala, amkumbuka mama yake kwa zawadi maalum

Muhtasari

•Harmonize amemzawadi mama yake kwa gari alipendalo aina ya Harrier siku chache tu kabla ya siku ya kusherehekea kina mama duniani.

•Siku ya Jumatano Harmonize alitangaza kuwa Range Rover ya pili ambayo alimnunulia mpenzi huyo wake wa zamani ingefika Ijumaa.

Harmonize na mama yake
Harmonize na mama yake
Image: HISANI

Baada ya kumfanyia makubwa aliyekuwa mpenziwe Fridah Kajala Masanja katika juhudi za kurejesha mahusiano yao, Harmonize sasa amemkumbuka mama yake pia.

Staa huyo wa Bongo amemzawadi mama yake kwa gari alipendalo aina ya Harrier siku chache tu kabla ya siku ya kusherehekea kina mama duniani.

Harmonize alionyesha gari mpya jeusi kwenye ukurasa wake wa Instagram na kufichua kuwa sio gari la kwanza kumnunulia mama yake.

"Mama Kondeboy hakuna gari anayoipenda zaidi ya Harrier. Usikute enzi ujana wake kuna mtu alimtesa kisa gari hii. Ndio maana hataki gari ya aina nyingine. Haya mama, hii hapa," Harmonize aliandika chini ya video ya  gari hilo.

Hatua hii inajiri baada ya ziara ya msanii huyo ya muziki nchini Kenya ambayo ilikabiliwa na changamoto chungu nzima.

Kondeboy amesema hakurudi Bongo mikono mitupu licha ya changamoto zote alizokutana nazo nchini Kenya ikiwemo kutiwa mbaroni.

"Hatimaye nimerudi na sikurudi mikono mitupu. Nimekuongeza hii nyingine  mama Kondeboy," Harmonize alisema.

Haya yalijiri siku moja tu baada ya bosi huyo wa Konde Music Worldwide kufichua kuwa amemwagizia mwigizaji Kajala gari jingine aina ya Range Rover.

Siku ya Jumatano Harmonize alitangaza kuwa Range Rover ya pili ambayo alimnunulia mpenzi huyo wake wa zamani ingefika Ijumaa.

"La pili siku ya Ijumaa. Lile jeusi kutoka Afrika Kusini tunalipia ushuru Goma, linakuja kupaki hapa. Kwa hivyo atakuwa na Range Rover mbili . ROVA demu wamuuni tuu sio kigogo Walekelini wala sio mke wa Laiza mchimba madini,"Alitangaza.

Harmonize alisema lengo lake ni kumfanya muigizaji huyo kuwa mwanamke ghali ambaye ataheshimika na wapenzi wake wote wa zamani.

"Niko na VX nyeupe na nyeusi kwa hivyo na yeye anaenda kuwa na mbili pia. Usafiri wa familia ulioje. Nataka nikufanye ghali mpaka maex waanze kukuita bosi washike na adabu bosi lady Kajala," Amesema.

Wiki kadhaa zilizopita mwanamuziki huyo alionyesha Range Rover nyingine ambayo alidai ni zawadi kwa Kajala.