Hatimaye Diana Marua akutana na mwanadada aliyechorwa tattoo ya sura yake na kumzawadi

Muhtasari

•Diana alimtembelea mwanafunzi huyo wa chuo cha urembo katika mtaa wa Githurai na kushiriki mazungumzo naye.

•Waithera alikiri kwamba alikosolewa sana baada ya kuchorwa tattoo hoyo ila anashikilia kuwa hana majuto yoyote kwa kile alichofanya.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Hatimaye mwanavlogu Diana Marua amepiga hatua ya kukutana na shabiki wake mkubwa ambaye alichora tattoo ya sura yake.

Rose Waithera alivuma mwezi jana baada ya picha za tattoo ya mke huyo wa Bahati aliyochorwa kwenye mgongo wake kuenea mitandaoni.

Diana aliwezwa na hisia baada ya kufikiwa na taarifa kuhusu kitendo cha mwanadada huyo na kumsihi ampatie 'muda wa kupumua'

""Sina maneno. Rose Waithera niruhusu nipumue kwanza," Diana alisema mwezi Machi.

Baada ya 'kupumua' kwa wiki kadhaa, Diana alimtembelea mwanafunzi huyo wa chuo cha urembo katika mtaa wa Githurai na kushiriki mazungumzo naye.

Waithera alisema aliamua kuchora tattoo ya mama huyo wa watoto wawili kwa kuwa anamshabikia sana na huwa anatamani kuwa kama yeye.

"Huwa napenda haiba yako., napenda sifa zako. Huwa natamani kuwa kama wewe. Uko na nyumba ya kifahari, uko na mume mzuri mwenye anakupamba kila wakati, uko na watoto wazuri. Sijawahi kupata mtu ako na roho kama yako. Ningependa kuwa kama wewe. Nakupenda," Waithera alimwambia Diana.

Mwanadada huyo alisema alianza mipango ya kuchorwa tattoo hiyo mwezi Desemba mwaka jana ila ikaja kuafikia miezi mitatu baadae.

Alikiri kwamba alikosolewa sana baada ya kuchorwa tattoo hoyo ila anashikilia kuwa hana majuto yoyote kwa kile alichofanya.

"Wengine walinitusi. Kwa wakati mwingine ningehisi vibaya. Ilifika wakati nikaona iko sawa. Sikuwahi kujuta," Alisema.

Diana alipungukiwa na maneno ya kumwambia mwanadada huyo katika mkutano wao ulioonyeshwa kwenye YouTube Channel yake.

Alimshukuru sana Waithera kwa upendo ambao alionyesha na kumuuliza kile ambacho angetaka kufanyiwa kama ishara ya shukrani.

Waithera aliomba kununuliwa vifaa vya kutengeza video na kulipiwa kodi ya nyumba, maombi ambayo Diana aliahidi kutimiza.

"Nitakununulia vifaa ambavyo unahitaji kutengeneza video, simu, stand ama chcochote utakacho nitakununulia. Nitalipa kodi ya nyumba, tutakubaliana ni kwa muda gani. Pia nitakulipia uende usome mambo ya makeup. Baada ya kusoma utatengeneza kazi yako na ujiajiri," Diana alimwambia Waithera.

Diana pia alimkabidhi Waithera zawadi zingine ambazo alikuwa amemnunulia njiani akielekea kwake.