•Jalas Junior alilalamika kuwa mbunge huyo katika siku za nyuma aliahidi kumsaidia lakini hakuwahi kutimiza ahadi hiyo.
•“Kwa hivyo ukiulizwa unafanya kazi gani kutafuta riziki.. Oooh nafanana na Jalas!” Jalas alihoji.
Siku ya Jumapili, Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o alijibu kwa utani baada ya mwanamume anayefanana naye kufanya mahojiano akilalamikia dhidi yake.
Jalas Junior, kama anavyojitambulisha kwenye mitandao ya kijamii, alilalamika kwenye mahojiano kuwa mtangazaji huyo wa zamani wa redio katika siku za nyuma aliahidi kumsaidia lakini hakuwahi kutimiza ahadi hiyo.
Blogu moja ya humu nchini ilichapisha mahojiano hayo kwenye mtandao wa Instagram na Jalang’o akajibu akisema kwamba hana jukumu la kumsaidia mtu kwa sababu tu anafanana naye.
“Mnajua nacheka nini? Hii ni maajabu! Yaani mkifanana sasa ukuwe wajibu wangu.. ungekuwa unafanana na mimi pia kwa kujituma na kutafuta haungefanya mahojiano haya!,” Jalang’o alijibu.
Mwanasiasa huyo aliendelea zaidi kuibua maswali kuhusu kazi ya kijana huyo akidokeza kwamba ‘kufanana na Jalas’ haiwezi kuwa kazi.
“Kwa hivyo ukiulizwa unafanya kazi gani kutafuta riziki.. Oooh nafanana na Jalas!” aliongeza.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, Jalas Junior alidai kuwa kitu pekee alichowahi kupata kutoka kwa mbunge huyo wa Lang’ata ni Ksh1000 baada ya kufanya naye mahojiano.
Alidai kuwa Jalang’o aliahidi kumsaidia baada ya mahojiano yao, lakini hajawahi kufanya hivyo licha ya yeye kumkumbusha mara kwa mara.
“Ujumbe wangu ni kumuuliza. Kwani alinidanganya?” Jalas Junior alihoji.
Kijana huyo amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii kwa muda sasa na amekuwa akifanya video za kumwiga mbunge huyo wa Lang’ata katika juhudi za kuunda maudhui.