•Alionyesha picha na video nzuri zake akishiriki muda na msichana huyo na kuziambatanisha na emoji za moyo kuonyesha upendo.
•Katika moja ya video alizochapisha, alionekana akicheza na binti yake na kumuonyesha jinsi ya kujiremba.
Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah hakuweza kuficha furaha yake alipotangamana na bintiye Keilah Oyando siku ya Jumapili.
Msanii huyo alipata nafasi adimu ya kukaa na mtoto huyo aliyempata na mwigizaji Caroline Muthoni, siku chache tu baada ya kukiri kuwa hajamwona kwa muda mrefu.
Alionyesha picha na video nzuri zake akishiriki muda na msichana huyo wa miaka mitatu na kuziambatanisha na emoji za moyo kuonyesha upendo.
Katika moja ya video alizochapisha, Mulamwah alionekana akicheza na binti yake na kumuonyesha jinsi ya kujiremba.
Keilah alizaliwa mnamo Septemba 2021, miezi michache tu kabla ya mchekeshaji huyo na mzazi mwenzake kutangaza kutengana. Wawili hao hata hivyo walikuwa wametengana miezi kadhaa kabla ya msichana huyo mrembo kuzaliwa.
Katika chapisho la mwezi uliopita, Mulamwah alidai kwamba alimuona binti yake mara ya mwisho akiwa na umri wa miezi minne pekee.
"Hakuna haja ya kwenda kwa Jeff na kusema 'Mulawah ana uhusiano mzuri na binti yake. Hakuna uhusiano... Sijamwona binti yangu. Nilimwona mara ya mwisho akiwa na umri wa miezi minne. Usifunike ukweli,” Mulamwah alisema.
Mchekeshaji huyo aliongeza kuwa yuko tayari kurekebisha mambo.
”Mmenitumia barua za mkitaka mtoto awekwe chini ya ulezi wa mtu mmoja pekee lakini hapa nje ninaitwa baba asiyewajibika. Kuna mengi. Isipokuwa sisi sote tutarahisisha, kila kitu kitapita... Nitadrive niende kwao, sijaenda huko miaka mingi. Ukiniona na mtoto ujue mambo ni sawa, kama sivyo.....” alisema.
Hivi majuzi, Mulamwah pia alifichua ni kwa nini alitoa taarifa ya kumkana binti huyo wake na Carrol Sonie miaka michache iliyopita.
Akiongea kwenye video iliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya Ruth K, mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alidai kwamba alichukua hatua hiyo kutokana na shinikizo kubwa lililokuwa likiendelea maishani mwake.
Alisema shinikizo lilianza kuongezeka kufuatia posti za mzazi mwenzake na mahojiano ambayo alifanya baada ya wao kutoa habari kuhusu kutengana kwao.
“Nilianza kukasirika, nikaanza kujibu kwa kupost vitu ambavyo sitakiwi kupost. Ninaamini Mungu kwamba alinishikilia, sikuposti kila kitu. Nimeshikilia vitu vingi sana ambavyo vikisemwa, vitaathiri vibaya maisha ya watu wengine, au vitachukuliwa vibaya," Mulamwah alisema.
Baba huyo wa watoto watatu alidai kuwa alitaka kuwafanya watu waache kumhusisha na mambo ambalo mzazi mwenzake alichapisha au kuzungumzia kwenye mahojiano.
“Nilipopost hivyo, nilitaka nibaki kando ya hii story ili wewe (Carrol) ukienda kwenye mahojiano mengine uongelee kuhusu mtoto wako, nisiwekwe kwa mix. Hilo lilikuwa wazo langu, baada ya hapo mambo ikaanza kuwa mingi,” alisema.