Hongera! Amber Ray na mpenziwe Kennedy Rapudo wanatarajia mtoto wa kwanza pamoja

Wawili hao walifichua habari hizo njema siku ya Jumatano asubuhi kupitia Instagram.

Muhtasari

•Amber Ray alichapisha picha nzuri inayomuonyesha mpenzi wake akiwa amemkamata kwenye kiuno huku mkono wake wa kushoto ukiwa umeshika kifaa cha kupima ujauzito. 

•Takriban miezi minne iliyopita, alifichua kuwa Jimal Rohosafi alimpachika ujauzito wakati walipokuwa kwenye ndoa.

Amber Ray na Kennedy Rapudo
Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mwanasosholaiti mashuhuri Faith Makau almaarufu Amber Ray amedokeza kuwa ana ujauzito wa mtoto wake wa pili.

Amber Ray na mchumba wake Kennedy Rapudo walifichua habari hizo njema siku ya Jumatano asubuhi kupitia Instagram.

Mama huyo wa mvulana mmoja alichapisha picha nzuri inayomuonyesha mpenzi wake akiwa amemkamata kwenye kiuno huku mkono wake wa kushoto ukiwa umeshika kifaa cha kupima ujauzito. 

"Oh Boy 🤭🤗 (Ewe mvulana)" aliandika chini ya picha hiyo.

Pichani, kulikuwa na vidokezo vingine vya mtoto anayekuja kama nguo ndogo ya mtoto na maandishi 'Oh baby'.

Wawili hao walipiga picha hiyo wakiwa jikoni na walionekana kuwa na furaha sana pamoja.

Haya yanajiri takriban miezi miwili tu baada ya wachumba hao wawili kuchumbiana rasmi jijini Dubai. Rapudo alimvisha Amber Ray pete ya uchumba wakati walipokuwa wameenda Dubai kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Amber Ray atakapojifungua, huyo atakuwa mtoto wake wa pili. Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 30 ana mtoto mwingine mvulana mwenye umri wa miaka 9 ambaye anaitwa Gavin.

Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na Kennedy Rapudo mapema mwaka jana, mama huyo wa mvulana mmoja alikuwa ameolewa na mfanyabiashara mashuhuri  Jimal Rohosafi kama mke wa pili.

Takriban miezi minne iliyopita, alifichua kuwa Jimal Rohosafi alimpachika ujauzito wakati walipokuwa kwenye ndoa.

Kwenye kipindi cha 'AS IT IS' kwenye YouTube Channel yake, Amber Ray alidokeza kuwa ndoa yake na Mwenyekiti huyo  wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu Nairobi yalianza kusambaratika baada yake kuwa mjamzito

"Hapo ndipo kila kitu kilipodhihirika kwani baada ya hapo ndipo alipopost mke wake na watoto. Nilihisi kama kuna kitu hakikuwa sawa," Amber Ray lisema katika mazungumzo na Shicco Waweru.

Mama huyo wa mvulana mmoja alieleza kuwa wakati alipokuwa akijitosa kwenye mahusiano na Jimal, mfanyibiashara huyo alikuwa amemhakikishia kwamba yeye na mkewe Amira walikuwa wakitalikiana.

"Mbona upost mtu ambaye unatalikiana naye? Nilikuwa napitia mengi," Alihoji.

Mwanasoshalaiti huyo alifichua kuwa ujauzito ambao alikuwa ameubeba haukutimia kwani uliharibika katika kipindi hicho.

Hata hivyo alidokeza kuwa hakujuta kuwa ilifanyika kwani hakuwa tayari kumlea mtoto ambaye angezaliwa pekee yake.

"Napendelea kuwa ilifanyika hivo kwani sidhani nitawahi kuwa na nguvu ya kuwa mama single katika maisha yangu kwani kwa hali nzima, hakuna njia ambayo tungeweza kuishia pamoja," Alisema Amber.