"Huru rasmi, tuondokeni wanangu!" Killy avunja rasmi uhusiano na Harmonize

Msanii huyo amedokeza kwamba tayari ametengeneza ngoma mpya chini ya usimamizi wake mpya.

Muhtasari

•Jumanne, Killy alitangaza kuwa yupo huru na tayari amepata usimamizi mpya baada ya kukatiza uhusiano na Harmonize.

•Usimamizi wa lebo ya Bongo ya Konde Music Worldwide ulitangaza kuondoka kwa Killy na  Cheed mapema mwezi jana.

Aliyekuwa msanii wa Konde Gang,Killy
Aliyekuwa msanii wa Konde Gang,Killy
Image: HISANI

Ni wazi kwamba mwimbaji wa Bongo Killy amemaliza rasmi kuondoka katika lebo ya Konde Music Wordwide.

Jumanne, Killy alitangaza kuwa yupo huru na tayari amepata usimamizi mpya baada ya kukatiza uhusiano na Harmonize.

Staa huyo wa Bongo pia amedokeza kwamba tayari ametengeneza ngoma mpya chini ya usimamizi wake mpya.

"Mungu ndiye mkuu  wa nyakati zote Walahhi. Huru rasmi sasa hivi. Alhamdulillah. Oya, wanangu jitayarisheni kwa kibao kipya," alisema kwenye Instastori.

"Video mpya za muziki, Usimamizi mpya, Pesa mpya, Kila kitu kipya. Lakini pia msisahau kujisajili kwenye YouTube Channel yangu inayojulikana kama "OfficialKilly". Tuondokeni wanangu muda wetu Huu!!"

Aidha, Killy tayari amefuta picha na video zote kwenye ukurasa wake wa Instagram. Huenda hatua hiyo inahusiana na kuondoka kwake.

Usimamizi wa lebo ya Bongo ya Konde Music Worldwide ulitangaza kuondoka kwa Killy na mwenzake Cheed mapema mwezi jana.

Bosi wa Kondegang, Harmonize aliweka wazi  kuwa lebo yake ilifikia makubaliano ya kutengana na wasanii hao wawili.

Konde Boy aliweka wazi kuwa wawili hao waliondoka kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wa lebo.

"Wasanii hawa watakuwa wasanii huru na kuweza kufanya kazi na kuingia mkataba na kundi au mtu yeyote na kuendeleza kazi zao kwani tunaamini ni vijana wasanii wenye uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika safari ya muziki," taarifa iliyotiwa saini na usimamizi wa Konde Music Worldwide ilisomeka.

Lebo hiyo ilibainisha haitahusika  na jambo lolote litakalohusisha wasanii hao kuanzia tarehe 10 Oktoba mwaka huu.

"Tunapenda kuwashukuru Killy na Cheed kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha kuwa pamoja na tunawatakia mafanikio mema katika kazi zao hapo baadae,"

Tetesi nyingi zilifuata baada ya kuondoka kwa wasanii hao.  Wawili hao walidaiwa kumshtaki Harmonize kwa madai ya kuwatimua.

Pia ilidaiwa kuwa wawili hao walikuwa wanatazamia kurejea kwa lebo yao ya zamani, Kings Music inayosimamiwa na Alikiba.

Killy na Cheed walijiunga na Konde Music Worldwide mwaka wa 2020 baada ya kugura kwenye lebo ya Alikiba ya Kings Music Records.