"Huwa anampiga kuua!" Akothee amnusuru mvulana anayedhulumiwa na mamake mwenye matatizo ya kiakili

Alifichua kuwa kijana huyo amevumilia mateso mengi kutoka kwa mama yake mzazi ambaye si mzima kiakili.

Muhtasari

•Mwanamuziki Akothee amemchukua mvulana mmoja wa shule ya msingi ambaye mama yake ana matatizo ya kiakili.

•Mwanamuziki huyo alionekana akimsaidia mvulana huyo wa Shule ya Msingi kuvaa sare zake.

 

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amemchukua mvulana mmoja wa shule ya msingi ambaye mama yake ana matatizo ya kiakili.

Mama huyo wa watoto watano mnamo Alhamisi alishiriki video ya kupendeza iliyomuonyesha akimsaidia mvulana huyo aliyetambuliwa kama Samson kujiandaa kwa ajili ya shule

Katika sehemu ya maelezo, alifichua kuwa Samson amevumilia mateso mengi kutoka kwa mama yake mzazi ambaye si mzima kiakili.

Mamake Samson ana matatizo ya kiakili. Hauwa anampiga kumuua wakati kichwa chake kinapoingia upande mwingine,” Akothee alisema kwenye taarifa.

Aliongeza, "Nimemchukua chini ya ulinzi wangu."

Katika video hiyo, mwimbaji huyo ambaye majuzi alizindua shule yake ya ‘Akothee Academy’ alionekana akimsaidia mvulana huyo wa Shule ya Msingi kuvaa sare zake.

Shule ya Akothee ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana ilianza kuchukua wanafunzi mwezi huu na mwimbaji huyo ameendelea kutoa wito kwa wazazi kuwapeleka watoto wao huko.

Mapema wiki hii, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alitangaza kuwa shule hiyo sasa imeanza kazi kutoka shule ya kulelea watoto wachanga hadi ya upili.

“Akothee Academy iko tayari na inafanya kazi. Imekuwa changamoto, lakini kwa neema ya Mungu, tumefaulu kuanzisha huduma za kulelea watoto na mapokezi. Madarasa ya PP1 na PP2 yanasimamiwa katika shule ya chini, wakati shule ya juu inachukua darasa la 1 hadi sekondari ya chini," alisema katika taarifa.

Aliongeza, “Mkabidhi mtoto wako kwetu, na tutawapa ujuzi wa kujitunza, kanuni sahihi za usafi, na kuwaunda kuwa watoa maamuzi wenye hekima. Ni muhimu kwamba tuwajibike kwa ajili ya jumuiya yetu, kwani familia imara huchangia jumuiya imara, ambayo nayo hujenga jamii yenye uthabiti. Jamii yenye uthabiti ni muhimu kwa taifa lenye ustawi, na msingi tunaotoa una jukumu muhimu katika hili."

Mwishoni mwa mwaka jana, mama huyo wa watoto watano alihitimu na shahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya.