Ibraah wa Kondegang atoroka baada ya kukabidhiwa maelfu ya pesa na Harmonize

Konde Boy alimtaja Ibraah kuwa msanii wake bora anayempenda sana.

Muhtasari

•Harmonize alisema anahitaji kupewa zawadi ya pesa kwenye siku yake ya kuzaliwa na si meseji tupu za heri ya kuzaliwa.

•Konde Boy alimtaja mwimbaji huyo wa kibao 'Nitachelewa' kama msanii wake bora ambaye anampenda sana.

Image: INSTAGRAM// IBRAAH

Siku ya Jumatano, Machi 15, bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 29.

Staa huyo wa wa bongo alipokea jumbe kutoka kwa watu wengi wakiwemo mashabiki na watu mashuhuri na pia akajitakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake, aliweka wazi kwamba anahitaji kupewa zawadi ya pesa kwenye siku yake ya kuzaliwa na si meseji tupu za heri ya kuzaliwa.

"Heri ya siku yangu ya kuzaliwa kwangu. Hili ndilo ua pekee ambalo ninahitaji maishani mwangu. Acheni kunitumia jumbe za heri ya siku ya kuzaliwa.  Ninazithamini lakini nahitaji ua kali kama hili," mwanamuziki huyo alisema kwenye video ambayo ilimuonyesha akiwa ameshika noti za pesa kwenye mkono wake.

Mikononi, alikuwa ameshika noti tano za dola mia moja za marekani, ambazo alimpa msanii wake Ibraah aliyekuwa amebarizi ndani ya gari lake. Dola mia tano ni takriban shilingi 64,900 za Kenya.

Konde Boy alimtaja mwimbaji huyo wa kibao 'Nitachelewa' kama msanii wake bora ambaye anampenda sana.

“Heri ya siku yako ya kuzaliwa kaka, ni siku yako ya kuzaliwa, sio yangu," alisema kabla ya kumwangushia Ibraah noti hizo.

Aliendelea kuahidi kuwekeza pesa nyingi kwa msanii huyo mwenye umri wa ujana ili aweze kupata pesa nyingi pia.

"Tuendelee Chinga. Kaka yangu nawekeza. Nataka mwakani uje unibariki kama hivi na mahela mengi sana," alimwambia.

Baada ya kupokea pesa hizo, Ibraah alirudi kwenye gari lake na kuondoka kabla ya mlinzi wa geti kufunga mlango.

"Sawa, Chinga anatoroka baada ya kupata pesa zake zote. Baada ya kukusanya pesa zake zote amekwenda. Pesa yangu inaenda ooh,"  Harmonize alisema kwa utani huku akimwangalia msanii huyo wake akiondoka.

Ibraah ambaye kwa jina halisi ni Ibrahim Abdallah Nampunga ndiye msanii pekee aliyesalia katika lebo ya muziki ya Harmonize ya Konde Music Worldwide. Wasanii wa zamani wa lebo hiyo, Killy, Cheed na Angella waliondoka katika kipindi cha miezi michache kati ya mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu.

Baada ya wasanii hao watatu kuondoka, Harmonize alimtia changamoto Ibraah kufanya muziki zaidi ili alete sifa kwa lebo.