"Imekuwa miaka 5 ya kukosa uhuru wangu!" Akothee alalamika

Muhtasari

•Akothee amefichua kwamba kwa kipindi cha takriban miaka mitano ambacho kimepita hajakuwa na uhuru wa kutembea mitaani.

•Ameeleza kuwa sasa imekuwa ngumu kwake kutembea jijini Nairobi kwa kuwa  Anayavutia macho ya wengi

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee ameweka wazi kuwa anazitamani sana siku ambazo hakuwa maarufu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amefichua kwamba kwa kipindi cha takriban miaka mitano ambacho kimepita hajakuwa na uhuru wa kutembea mitaani.

Ameeleza kuwa umaarufu wake mkubwa umefanya hata iwe vigumu kwake kuendesha gari jijini Nairobi.

"Wakati ambao bado ningeweza kutembea kwa uhuru katika CBD, Sasa hata huwa siendeshi gari huko. Imekuwa miaka mitano ya kukosa uhuru wangu," Akothee alisema.

Alikuwa anazungumzia kumbukumbu yake ya miaka kadhaa iliyopita wakati binti yake mkubwa Vesha Okello alikuwa katika shule ya upili.

Mama huyo wa watoto watano alipakia picha yake na binti huyo wake wakitembea pamoja jijini Nairobi.

"Huyu ni mimi na binti yangu wa kwanza @veshashaillan tukielekea kwa benki kulipa karo ya shule baada ya kupata kiamsha kifungua kinywa nzito katika hoteli ya Stanley Nairobi," Akothee aliandika chini ya picha hiyo.

Ameeleza kuwa sasa imekuwa ngumu kwake kutembea jijini Nairobi kwa kuwa  Anayavutia macho ya wengi kutokana na umaarufu wake.

Aidha mwanamuziki huyo amewasherehekea watoto wake watano huku akiwataja kama "maisha yangu."

Akothee alijitosa kwenye taaluma ya muziki zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alijizolea umaarufu mkubwa kati ya mwaka wa 2014-2016.

Taaluma ya mwanamuziki huyo ambaye pia ni mfanyibiashara imezingirwa na utata mwingi kutokana na mtindo wake wa maisha.

Akothee anaaminika kuwa miongoni mwa wasanii tajiri zaidi nchini Kenya na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki.