Jamaa aliyehusishwa na CAS Millicent Omanga hatimaye avunja kimya

Robbie aliweka wazi kwamba alipiga picha za kawaida tu naye miaka michache iliyopita.

Muhtasari

•Katika taarifa ya Jumatano, Robbie alitupilia mbali ripoti zinazomhusisha kimapenzi na seneta huyo wa zamani.

•Robbie alilalamika kwamba kitendo cha gavana huyo wa zamani kutumia picha zake kusimulia simulizi yake kimemharibia jina.

Image: HISANI

Robbie Mediskah Njama, kijana ambaye alishutumiwa kwa kusambaza picha na video za uchi zinazodaiwa kuwa za CAS Millicent Omanga hatimaye amevunja ukimya wake.

Katika taarifa ya Jumatano, Robbie alitupilia mbali ripoti zinazomhusisha kimapenzi na seneta huyo wa zamani huku akiweka wazi kwamba alipiga picha za kawaida tu naye miaka michache iliyopita.

Njama alimkashifu  gavana wa zamani wa Nairobi, Mike Sonko kwa kumhusisha kimapenzi na Omanga kwa kuchapisha picha za kumbukumbu zao.

"Nilifahamu jana usiku kwamba Mike Sonko Mbuvi, aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter uliokuwa na picha yangu na CAS wa Mambo ya Ndani Millicent Omanga akisisitiza kwamba mimi ni raia wa Tanzania ambaye ako nyuma ya picha na video za CAS Millicent zilizopakiwa hivi majuzi,” alisema.

Aliendelea, "Kwa hivyo ninachagua kushughulikia simulizi kama kuharibiwa jina kwa sababu picha hizo mbili ni za 2017-2019.”

Mwanahabari huyo pia alimkosoa gavana huyo wa zamani kwa kumhusisha na picha zake  zilizohaririwa akiwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Rachel Shebesh.

“Watu wanaonijua ana kwa ana wanaweza kubaini hadithi hii kama uwongo na wengi wao wananiheshimu sana,” alisema.

Robbie alilalamika kwamba kitendo cha gavana huyo wa zamani kutumia picha zake kusimulia simulizi yake kimemharibia jina.

"Kama mtu ambaye anafurahia haki yake katika ardhi hii, sitaiacha iteleze, na Mike Sonko anapaswa kujibu maswali yangu kwa sababu ukweli, mbali na kuharibu sura yangu hadi sasa, imeniathiri kisaikolojia na pia wale walio karibu nami. Kutumia picha zangu kuchafua jina langu sio tu kudhoofisha, bali pia ni makosa," alisema.

Alibainisha kuwa yeye ni kijana mwenye mustakabali mzuri mbeleni na kuweka wazi kwamba madai kama hayo yanaweza kuwa na madhara kwa hatua zake za siku zijazo.

Aidha, alimpa pole CAS Omanga kwa masaibu yaliyompata na kumtaka awe na ujasiri katika kipindi hiki cha majaribu.

“Nachukua nafasi hii kumtia moyo Mhesh Omanga kwa sababu kipindi hiki lazima kiwe kizito kwake na kwa familia yake pia .Uwe jasiri Mhesh. Jamani, nina nguvu na lazima mtu alipe kwa hili. Asanteni wote,” alisema.

Hivi majuzi, video ya mwanamke aliye uchi iliyorekodiwa wakati usiothibitishwa ilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya Wakenya wakidai mhusika ni CAS Omanga. Walakini, hakuna kilichothibishwa kufikia sasa.

Siku ya Jumanne, Mike Sonko aliibua madai kwamba Robbie ndiye aliyehusika kusambaza picha za mwanasiasa huyo.