Je, Zuchu anachubua ngozi yake? - Mama yake aweka mambo wazi

Staa huyo wa Taarab ameweka wazi kuwa watoto wake wawili walizaliwa wakiwa weupe.

Muhtasari

•Kumekuwa na tetesi kuwa Zuchu amekuwa akijaribu kujibadilisha tangu alipojizolea umaarufu mkubwa baada ya kujiunga na WCB.

•Khadija Kopa alibainisha kuwa bintiye amekuwa na ngozi nyeupe katika siku zote za maisha yake.

Khadija azungumzia suala la bintiye Zuhura kuolewa
Khadija azungumzia suala la bintiye Zuhura kuolewa
Image: HISANI

Staa mkongwe wa Taarab, Khadija Kopa amezizima tetesi kuwa binti yake Zuhura Othman almaarufu Zuchu amekuwa akichubua ngozi yake.

Katika mahojiano na Mbengo TV, Kopa alibainisha kuwa bintiye amekuwa na ngozi nyeupe katika siku zote za maisha yake.

Aliweka wazi kuwa watoto wake wawili walizaliwa weupe ilhali wengine wawili waliibuka kuwa weusi.

"Zuhura hivyo alivyo yuko vile. Zuhura mweupe tangu alipozaliwa, yeye na kakake marehemu Omari. Watoto wangu walikuwa wawili weupe na wawili weusi," Bi Kopa alisema.

Malkia huyo wa mipasho alisema hakuna uwezekano kuwa Zuchu anajichumbua ngozi na kudai kuwa picha za mitandaoni zinazoonyesha akiwa mweupe zaidi huenda zimefanyiwa ukarabati kutumia kompyuta.  

"Yuko vilevile. Ukiona picha kwenye simu labda kukarabati kutumia filter. Lakini uso yuko vile. Rangi yake ile. Hajichubui," Alisema.

Kumekuwa na tetesi kuwa Zuchu amekuwa akijaribu kujibadilisha tangu alipojizolea umaarufu mkubwa baada ya kujiunga na WCB.

Malkia huyo kutoka Zanzibar alisajiliwa na Diamond kwenye lebo hiyo yake mwakani 2020 na umaarufu wake umeendelea kukua kila uchao.

Imedaiwa kuwa mtunzi huyo wa kibao  'Sukari' amekuwa akijaribu kujifanyia marekebisho kadhaa ikiwemo ya ngozi yake ili kukabiliana na umaarufu.

Zuchu pia amedaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na bosi wake Diamond, madai ambayo yamekithiri mwaka huu.

Mwezi uliopita Diamond kwa mara ya kwanza alijitambulisha hadharani kama mume wa malkia huyo kutoka Zanzibar.

"Huyo ni mume wa Zuuh," Alijibu chini ya video iliyomuonyesha akitumbuiza mashabiki wake nchini Ureno.

Siku chache baadae hata hivyo Zuchu alikana kuwa yeye ndiye aliyekuwa anazungumziwa na bosi huyo wake.

"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alijibu katika mazungumzo ya simu na mtangazaji wa Wasafi Media alipohojiwa kuhusu matamshi ya Diamond.

Katika mazungumzo hayo, Binti huyo wa Khadija Kopa bado alisistiza kuwa  uhusiano wake na Diamond ni wa kikazi.