Jinsi DJ Mo na Size 8 walivyopatanishwa baada ya kutengana kwa muda

Size 8 alidokeza kuwa alikubali kumsamehea mumewe baada ya kukiri kosa lake na kuomba msamaha.

Muhtasari

•Wanandoa hao walifichua kuwa watumishi wa Mungu waliwasaidia kupatana na kurudisha familia yao pamoja.

•Walichua  kuwa  baadhi ya marafiki wa familia akiwemo mwimbaji  Daddy Owen na Director Richie pia walihusika katika upatanisho.

Image: INSTAGRAM// DJ MO

Jumatano, wanandoa mashuhuri DJ Mo na Size 8 hatimaye walijitokeza kueleza hali halisi ya ndoa yao iliyodaiwa kusambaratika.

Ripoti za matatizo katika ndoa ya wasanii hao  zilisambaa wikendi iliyopita baada ya kufichuliwa na vyombo mbalimbali vya habari.

Katika video waliyochapisha kwenye YouTube, Size 8 alikiri kuwa alikuwa amekimbia nyumba yake ya ndoa na kumuacha mumewe. Aliweka wazi kuwa alikuwa amegura ndoa yake  baada ya mumewe  DJ Mo kumkosea vibaya.

"Ndio nilitoroka. Nilikuwa nimemkasirikia sana DJ Mo. Alinikosea. Nilihitaji tu nafasi yangu niweze kupumua na kuongea na Mungu kwa kuwa naamini nikiwa na hasira na tuko kwa nyumba moja tutaongeleshana vibaya na kufanyiana vibaya," Size 8 alisema huku akiwa amesimama sako kwa bako na mumewe.

Ripoti za awali zilikuwa zimedokeza kuwa juhudi nyingi  za kuwapatanisha hazikuzaa matunda  kwani Size 8 alikuwa na hasira sana na mumewe. Vyanzo vya habari vilisema mwimbaji huyo aliwaomba marafiki na wanafamilia waliojaribu kuwapatanisha kumpa muda wa kufikiria kuhusu ndoa yao.

Wanandoa hao walifichua kuwa watumishi wa Mungu waliwasaidia kupatana na kurudisha familia yao pamoja.

"Tuliketi chini na Pastor Joan na Pastor Chris Chege na tukafikia hitimisho na ufahamu wa kibiblia na sasa tumepatanishwa tena kwenye ndoa kwa sababu ya neema na rehema za Mungu," Alisema.

Walichua  kuwa  baadhi ya marafiki wa familia akiwemo mwimbaji  Daddy Owen na Director Richie pia walihusika katika upatanisho wao.

Size 8 alidokeza kuwa alikubali kumsamehea mumewe baada ya kukiri kosa lake na kuomba msamaha.

"Kitu kizuri na Mo ni kuwa Mo alikubali kosa lake na kuomba msamaha. Tulishiriki kikao na watumishi wa Mungu na tukabarikiwa na walichotuambia na jinsi Yesu alivyotupatia mwelekeo," Alisema .

Alisema kuwa kipindi alichokuwa amekimbia ndoa yake na kuwabeba watoto wao Ladasha Wambui na Samuel Muraya Jr, wawili hao walitamani sana kurudi nyumbani na hata kumuuliza ingefanyika lini. 

"Ukweli ni kuwa ilitokea na ni jambo la kawaida kwa ndoa," Size 8 alisema.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa ndoa ya wawili hao kutikisika. Mwaka wa 2020, aliyedaiwa kuwa mchepuko wa DJ Mo alifichua mazungumzo na matukio yake ya karibu na mcheza santuri huyo kupitia mwanablogu Edgar Obare.

Baadae wanandoa hao walifanya amani kwenye kipindi chao cha 'Dining with the Murayas' baada ya kile walichokiita 'Wiki ya masaibu'.