Juliani apewa mboga za kienyeji baada ya kukiri kuwa amesota

Rapa huyo alipokea aina tofauti za mboga kutoka kwa mashabiki wake.

Muhtasari

•Mzazi huyo mwenza wa Lilian Nganga alionekana akipokea terere, managu, majani ya muhogo na sukumawiki.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya rapa huyo kukiri kuwa hayuko katika hali nzuri ya kifedha kwa sasa.

Mwimbaji Juliani apokea mboga kutoka kwa shabiki
Image: HISANI

Wikendi mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za kufoka Julius Owino almaarufu Juliani alizawadiwa mboga za asili.

Juliani ambaye kwa muda wa siku kadhaa ambazo zimepita amekuwa akitamba baada ya kukiri hadharani kuwa anapitia changamoto za kifedha alipokea aina tofauti za mboga kutoka kwa mashabiki wake.

Katika video iliyofikia Radio Jambo, mzazi mwenza huyo wa aliyekuwa mke wa mwanasiasa Alfred Mutua, Lilian Nganga alionekana akipokea terere, managu, majani ya muhogo na sukumawiki.

"Mpishi achanganye zote. Ipikie hivyo tu vile imekuja..," alishauriwa na shabiki aliyemkabidhi mboga hizo.

Mashabiki ambao walimzawadia Juliani mboga walikuwa na rasta kama yeye. Kwa kawaida warasta huwa ni wapenda mboga kwani wengi wao ni walaji mboga tu na huwa wanakwepa nyama.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya rapa huyo kukiri kuwa hayuko katika hali nzuri ya kifedha kwa sasa.

Katika taarifa ya video aliyotoa Jumatano ya wiki iliyopita, Juliani hata hivyo alibainisha kuwa bado hajafilisika.

Alieleza kuwa changamoto zinazomkabili zimetokana na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ametumia kwenye miradi yake katika siku za nyuma.

"Katika miaka mitatu iliyopita nimekuwa nikiweka pesa zangu kwa kila kitu nilichofanya. Sina wafadhili, sina wawekezaji, sina chochote. Nimeweka pesa zangu kidogo kwa ajili ya hayo," alisema katika video aliyopakia Twitter.

Rapa huyo alidokeza kwamba hata alichukua madeni kadhaa katika juhudi za kukamilisha baadhi ya miradi yake.

Aidha alifichua kuwa changamoto za kifedha zinazomkabili kwa sasa zimesababisha yeye kukosa muda wa kuwa mwanawe huku akimshukuru mkewe na mzazi mwenzake Lilian Nganga kwa kumuelewa.

"Siwezi kupata muda na mwanangu sasa kwa sababu nahangaika huku na kule nikijaribu kulipa madeni niliyochukua ili kutimiza mambo kadhaa ambayo nilijiahidi kutimiza. Namshukuru sana mama (Lilian) kwa kuelewa ninachojaribu kufanya," alisema.

Juliani hata hivyo alibainisha kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto za kifedha bado hajafilisika kwani angali anaweza kukidhi mahitaji muhimu.

"Mkiniona nikihangaika sifanyi, sifanyi hayo yote kwa ajili yangu mwenyewe. Niko sawa , kuna paa juu yangu naweza kujilisha lakini niko na ndoto zangu," alisema.

Alitaja baadhi ya maazimio yake kuwa kutengeza nafasi 10,000 za kazi, kupatia wasanii mikopo na kuachilia muziki zaidi. Alisema kuwa amejipatia miaka 10 kutimiza ndoto aliyo nayo kwa jamii yake.

"Pesa ambazo nimekuwa nikiwekeza miaka mitano iliyopita hazijaleta faida bado," alisema.

Pia alieleza kusikitishwa kwake na watu wanaofanya mzaha kuhusu hali yake ya sasa na kuwaomba wakome kuendelea.