Kajala aghadhabika baada ya mtetezi wa Harmonize kukosoa gauni lake, amuita mke mwenzake

Kajala alimtaka mtangazaji huyo kuachana na maisha yake.

Muhtasari

•Mwijaku alikosoa gauni ambalo Kajala alivalia kwenye hafla ya mwimbaji Marioo iliyofanyika wiki jana.

•Kajala alidokeza kwamba gauni lake ni ghali, kinyume na alivyosema Mwijaku kwamba ni la mtumba.

Kajala Masanja na Mwijaku
Image: INSTAGRAM

Muigizaji mkongwe wa filamu Bongo Frida Kajala Masanja amechoshwa na ukosoaji na kumjibu mtangazaji mashuhuri,  Mwijaku.

Hivi majuzi, Mwijaku ambaye amejitwika jukumu la kumtetea bosi wa Kondegang, Harmonize na washirika wake alikosoa gauni ambalo Kajala alivalia kwenye hafla ya mwimbaji Marioo iliyofanyika wiki jana.

"Angalia gauni alilovaa. Mpaka watu wanacomment wanasema Harmonize alikuwa na moyo kama huo mzigo ndo alikuwa anashinda nao mpaka kwenye Gym. Angalia nguo alilovaa katika sehemu kama ile alafu unapanda kwenye steji nguo inaonyesha viungo vyako vyote. Hakupaswa kuvaa nguo kama ile, hafla hiyo ilikuwa imehudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi," Mwijaku alisema kwenye mahojiano na Carrymastory.

Mchekeshaji huyo aidha alidai kwamba gauni la muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 lilikuwa la mtumba.

Alisema kutokuwa na mume ndiko kulikopelekea Kajala kuvaa vile na kueleza jinsi alivyosikitishwa naye.

"Wakati alikuwa na Harmonize, hungemuona na kitu kama kile. Alikuwa anavaa kupendeza," alisema.

Mwijaku pia alichukua fursa hiyo kuwapongeza wasanii Hamisa Mobetto na Wema Sepetu kwa jinsi walivyovalia usiku huo.

Huku akijibu kwenye ukurasa wake wa Instagram, Kajala alimtaka mtangazaji huyo kuachana na maisha yake.

Mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba gauni lake ni ghali, kinyume na alivyosema Mwijaku kwamba ni la mtumba.

"Kuna mke mwenzangu huko anahangaika na gauni langu, mwambieni aende @beautypointdar atajua bei," alisema.

Kajala ameonekana huru na mwenye furaha sana baada ya kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana.

Wawili hao ambao walirudiana mwezi Mei walikuwa wamechumbiana kwa miezi kadhaa na hata kudokeza harusi kabla ya kuachana katika hali isiyoeleweka. Hakuna yeyote kati yao ambaye ameeleza kilichotokea.

Mwijaku alikuwa amesitisha urafiki na Harmonize baada ya kujitosa kwenye mahusiano na Kajala na hata kuanza kufanya kazi na hasidi wake Diamond Platnumz. Hata hivyo, tayari ametangaza kurejea kwake katika Kondegang baada ya mahusiano hayo kusambaratika Desemba mwaka jana.