"Grow some balls!" Karen Nyamu atoa changamoto kwa Samidoh kumuunga mkono

Muhtasari

•Karen alimpa changamoto baba ya watoto wake wawili, mwanamuziki Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kumuunga mkono  katika kampeni zake

•Alisema kwamba kwa sasa anataka kuweka maisha yake ya kibinafsi kuwa siri na kuangazia siasa zake.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU, SAMIDOH

Mwanasiasa na wakili mashuhuri Karen Nyamu ameeleza imani yake kubwa katika kunyakua kiti cha Useneta wa Nairobi.

Akihutubia wanahabari katika tamasha iliyoandaliwa Jumamosi usiku kwa minajili ya kuchangisha bili ya hospitali ya Akuku Danger, mama huyo wa watoto watatu aliwaomba wakazi wote wa Nairobi kumuunga mkono katika azma yake.

Karen alimpa changamoto baba ya watoto wake wawili, mwanamuziki Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kumuunga mkono  katika kampeni zake. Alisema utakuwa uamuzi wa Samidoh iwapo anataka kuhusika  au la.

"Ni uamuzi wake binafsi. Mnajua anapenda kutoka hiyo stori na kuihepa. Sijui, ni yeye ataamua kama atapata hizo 'balls'," Karen alisema.

Hata hivyo ,Karen alidokeza kuwa angependa kuona  mzazi huyo mwenzake akiwa katika mstari wa mbele kumpigia debe.

Mwanasiasa huyo alisusia kuzungumza kuhusu suala la Samidoh  kuhusika katika malezi ya watoto wao wawili.

Alisema kwamba kwa sasa anataka kuweka maisha yake ya kibinafsi kuwa siri na kuangazia siasa zake.