Kunani? Mkewe Samidoh, Edday Nderitu azua wasiwasi mkubwa kuhusu ndoa yao ya miaka 15

Edday ameacha kumfuatilia mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi kwenye mtandao wa Instagram.

Muhtasari

•Mwimbaji Samidoh si miongoni mwa akaunti 524 ambazo Bi Edday Nderitu anafuatilia kwenye mtandao wa Instagram.

•Mwezi Februari, Edday alimuonya Samidoh kwamba hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. 

amezua wasiwasi kuhusu ndoa yao ya miaka 15.
Mkewe Samidoh, Edday Nderitu amezua wasiwasi kuhusu ndoa yao ya miaka 15.
Image: HISANI

Mkewe Samidoh, Bi Edday Nderitu amezua wasiwasi mkubwa kuhusu ndoa yao ya zaidi ya mwongo mmoja baada ya kuacha kumfuatilia mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi kwenye mtandao wa Instagram.

Haijabainika ni lini mama huyo wa watoto watatu alichukua hatua ya kuacha kumfuatilia mzazi huyo mwenzake lakini uchunguzi wetu katika ukurasa wake wenye zaidi ya wafuasi elfu tisini umebainisha kwamba mwimbaji huyo si miongoni mwa akaunti 524 ambazo anafuatilia kwenye mtandao huo wa kijamii. 

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya yeye kufunga safari ya ndege kuelekea marekani pamoja na watoto wake watatu. Bado hajathibitisha kama alirejea nchini Kenya na kama bado, wakati anapanga kufanya hivyo.

Image: INSTAGRAM// EDDAY NDERITU

Hii sio mara ya kwanza kwa Edday Nderitu kuzua wasiwasi kuhusu ndoa yake na mwanamuziki huyo wa Mugithi. 

Takriban miezi miwili iliyopita, mama huyo wa watoto watatu alizua tetesi za kuvunjika kwa ndoa yao ya miaka kumi na mitano baada ya kushiriki katika challenge ya Tiktok  ya wimbo wa Harmonize ‘Single Again.’ 

Edday alichapisha video fupi iliyomuonyesha akiwa amelala peke yake kwenye kochi huku akigugumia maneno ya wimbo huo mpya wa Konde Boy. Kwenye video, alionekana huru na mwenye furaha huku akiimba;-

"Maybe this love is not for me,

I am single,

Do you know that I am single?

I am single again," aliimba.

Kumaanisha, {"Labda mapenzi haya sio yangu, niko single, Je, unajua kuwa niko single?, niko single tena."}

Baadhi ya mashabiki waliotoa maoni walionekana kusoma ujumbe huo kama tangazo kwamba hayuko tena na Samidoh.

Wawili hao hata hivyo walionekana pamoja mara kadhaa baadaye hadi mapema mwezi huu wakati Edday aliondoka nchini.

Mnamo mwezi Februari, Bi Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. Hii ilikuwa baada ya msanii huyo kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya awali kudaiwa uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.