Lebo ya Diamond WCB kusajili wasanii wapya licha ya kushtumiwa kwa kuwanyonya

Fella alisisitiza kuwa lengo la WCB ni kusaidia msanii kukua na kupata kitu kutoka kwa muziki wao.

Muhtasari

•Mkubwa Fella amesisitiza kuwa lebo hiyo itaendelea kuwasaini wasanii wengine wapya licha ya ukosoaji mkubwa ambao wamekumbana nao katika siku za hivi majuzi.

•Fella alithibitisha kuwa mikataba ya lebo hiyo inaelekeza msanii kupata 40% pekee na kubainisha kuwa pesa zinazosalia hutumika kulipa mishahara na kugharamia utayarishaji na uuzaji wa muziki.

Diamond Platnumz na meneja wa WCB Mkubwa Fella
Image: INSTAGRAM// MKUBWA FELLA

Mmoja  wa mameneja wa WCB, Mkubwa Fella, amesisitiza kuwa lebo hiyo itaendelea kuwasaini wasanii wengine wapya licha ya ukosoaji mkubwa ambao wamekumbana nao katika siku za hivi majuzi.

Kipindi fulani kilichopita, wadau kadhaa katika tasnia ya muziki wa Bongo walijitokeza na  kuishutumu lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz kwa kuwakandamiza na kuwanyonya wasanii wake.

Meneja huyo hata hivyo amepuuzilia mbali ukosoaji huo na kusema kuwa lengo la WCB ni kusaidia msanii kukua na kupata kitu kutoka kwa muziki wao, kinyume na tetesi zilizoibuliwa hapo awali.

"La msingi,je maneno yatatusababishia tuache kuwasaidia watu? Hakuna! Sisi tutasaidia watu, maneno yapo hadi tutakapokufa kutakuwa na maneno," Mkubwa Fella alisema katika mahojiano na Mbengo TV.

Aliwasuta wakosoaji wao huku akibainisha kwamba huwa wanajitokeza wakati tu msanii tayari ameshaimarika na huwa hawaonekani wakati msanii huyo anapokuwa akifanyiwa kazi ili kuwa bora.

"Msanii akifanikiwa unamuona mjombake, babake, shangazi yake na nani wake. Unakuja kuambiwa ati unamdhulumu mpaka unaonekana ni kama utakuja kukata tamaa. Lakini bado tusaidiane na tuendelee, maneno yapo. Kama sisi wenyewe tumeamua kujenga kwenye jalala, utakataa uvundo? Lazima inuke," Alisema.

Siku kadhaa zilizopita wadau kadhaa katika tasnia ya muziki wa Bongo wakiongozwa na mtayarishaji maarufu P-Funk Majani walikosoa lebo ya WCB na kuwashtumu wasimamizi wake kwa kukandamiza Wasanii.

Baadhi ya wadau walikosoa sera ya WCB ya kuchukua 60% ya kipato wanachoingiza wasanii wake na kuwapatia asiliamia 40  tu.

Katika mahojiano ya awali, Fella alithibitisha kuwa mikataba ya lebo hiyo inaelekeza msanii kupata 40% pekee na kubainisha kuwa pesa zinazosalia hutumika kulipa mishahara na kugharamia utayarishaji na uuzaji wa muziki.

"Mi nilichungulia kuna mkataba mmoja una 40% kwa 60%. Asilimia 40  ni za msanii kutumia na ndugu zake. Asilimia 60 kuna meneja, kuna mkurugenzi lakini bado kuna hela ya kusaidia muziki wa yule msanii maanake kuna kurekodi, kuna kufanya video, kuna kurekodi, kuna promotion.. vitu vyote vinafanyika kwa mwendo huo," Mkubwa alisema katika mahojiano ya awali na Wasafi Media.

Meneja huyo mkongwe pia alidokeza kuwa wasanii  wengi wamekuwa wakigura WCB katika juhudi za kushindana na Diamond.