Malezi kisasa! Zari na wanawe waonekana wakiburudika pamoja, kubugia mvinyo na kuvuta shisha (+picha)

Mwanawe Zari, Pinto Tale alisherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumatatu, Agosti 8.

Muhtasari

•Zari alionyesha klipu za video na picha zake na wanawe katika kilabu cha kifahari ambapo walionekana kuwa na wakati mzuri.

•Huku akimtakia heri ya siku ya kuzaliwa mwanawe Pinto Tale , Zari Hassan alimhakikishia upendo wake mkubwa kwake.

pamoja na wanawe Pinto Tale na Raphael Ssemwanga.
Zari Hassan pamoja na wanawe Pinto Tale na Raphael Ssemwanga.
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Siku ya Jumatatu, mwanasholaiti na mfanyabiashara maarufu wa Uganda  Zari Hassan alionekana akiburudika katika kilabu pamoja na wanawe wawili wakubwa Pinto Tale na Raphael Ssemwanga Jr

Katika ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano alionyesha klipu za video na picha zake na wanawe katika kilabu cha kifahari ambapo walionekana kuwa na wakati mzuri.

Katika video hizo, watatu hao ambao pia walikuwa pamoja na marafiki wengine wa wanawe Zari walionekana kuwa na furaha nyingi na tabasamu kwenye nyuso zao zilidhihirisha hilo

Katika video moja,  Zari alionekana akibugia glasi ya mvinyo huku mwanawe mkubwa, Pinto Tale akirekodi matukio hayo ya kufurahisha kwa kutumia kamera ya simu. Video nyingine ilimuonyesha Raphael akivuta moshi wa shisha huku mama yake akiwa amemshika kwenye bega.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Zari kuonekana na wanawe klabuni hapo, katika siku za nyuma aliwahi kuandamana nao kwenda kujiburudisha kwenye vilabu mbalimbali na kisha kurekodi matukio hayo kwenye mitandao ya kijamii.

Mwanawe Zari, Pinto Tale alisherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumatatu, Agosti 8.

Huku akimtakia mwanawe heri ya siku ya kuzaliwa, mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz alimhakikishia upendo wake mkubwa kwake.

"Heri ya kuzaliwa Pinto Tale. Kijana, inaonekana wewe si shabiki wa shots moja. Nakupenda kido,” Zari alimwandikia mwanawe, Pinto Tale kwenye Instagram.

Ni mara nyingi ambapo mfanyibiashara huyo anayeishi Afrika Kusini ameonekana akijumuika na Pinto Semwanga ,20,  na Raphael  Semwanga ,17, kujivinjari pamoja na marafiki zao kwenye maeneo mbalimbali ya burudani. 

Hii ni moja tu ya viashirio vingi vinavyoonyesha kuwa mwanasoshalaiti huyo ana uhusiano wa karibu sana na watoto wake.

Kujivinjari pamoja na wanawe bila kuzingatia pengo kubwa kati ta umri wake na wao sio jambo la kawaida hasa barani Afrika.

Kando na hilo, Zari ameonekana kuwa tofauti sana na wazazi wengi wa Kiafrika kuhusu jinsi ya kusimamia mali na biashara za familia.

Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 amewaaminia  kwa kiwango kikubwa wanawe wakubwa  na usimamizi wa biashara  na mali  nyingi iliyoachwa nyuma na aliyekuwa mumewe marehemu Ivan Semwanga.

Mapema mwaka jana, Zari alianzisha mchakato wa kuhamisha uongozi wa Chuo cha Brooklyn City kwa watoto wake.

Mnamo mwezi Januari 2022, mzaliwa huyo wa Uganda alitumia ukurasa wake wa Instagram kutangaza kuwa amemteua mwanawe mkubwa Pinto Ntale kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Chuo hicho.

"Mkurugenzi Mtendaji Mkuu. mafunzo, wafundishe wangali vijana, siwezi kusubiri kumwona akichukua kampuni na kusimamia fedha,” Zari alisema.

Lingine linalomtofautisha Zari na wazazi wengine ni jinsi anaendeleza ushirikiano mzuri katika malezi na mzazi mwenzake Diamond Platnumz.