•Mama Dangote hata hivyo ameweka wazi kuwa hivi majuzi hajamfuata wala kum-unfollow mtu yeyote kwenye Instagram.
•Mama Dangote ameweka wazi kuwa Tanasha Donna alimpa zawadi ghali kwa niaba ya mtoto wake Naseeb Jr.
Mama mzazi wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu kama Mama Dangote amekanusha madai ya kugombana na msanii wa WCB Zuchu ambaye anadaiwa kuwa mpenzi na mwanawe.
Tetesi za mzozo kati ya Mama Dangote na Zuchu ziliibuka siku ya Alhamisi baada ya mama huyo wa Diamond kudaiwa kum-unfollow malkia huyo wa bongo fleva kwenye mtandao wa Instagram. Pia alidaiwa kukubaliana na maoni ya shabiki mmoja aliyependekeza Diamond kurudiana na Tanasha na kumtimua Zuchu.
Wakati akijibu tuhuma hizo, Mama Dangote hata hivyo aliweka wazi kuwa hajamfuata wala kum-unfollow mtu yeyote kwenye Instagram hivi majuzi.
“Mimi wasije wakaniingiza kwenye mambo yao. Mimi sijamu-unfollow. Niliowa-follow hao hamsini, ndio hao hao hamsini. Sasa nimuunfollow kwa kipi?” Mama Dangote aliiambia Wasafi Media.
Aliongeza, “Mimi mwenyewe ata nikigombana na mtu atajua mwenyewe. Niliowa-follow ni hao hamsini ,sina hamsini na moja. Mambo ya kitoto ya zamani wasiniingize. Mimi najijua mtu mzima. Mimi nimuunfollow amenifanya nini?”
Mama Diamond pia alikanusha madai ya ku-pin maoni ya mtumizi wa Instagram ambaye alidai kuwa Tanasha Donna ndiye mke sahihi wa bosi huyo wa WCB na kupendekeza kuwa ni wakati wa yeye kumtimua Zuchu na kumfanya awe kicheko.
“Wanasema eti mimi nime-pin comment. Ni nini? Simu ya iPhone sijui kutumia. Nimegusa labda kimakosa. Jana (Jumatano) simu sikuwa nayo, nilikuwa na wageni. Nimegusa saa ngapi? Kupost kwenyewe siposti. Kassim ndiye ananipostia, mimi siwezi nimepewa tu simu iPhone na Naseeb. Siwezi,” alisema Mama Dangote.
Mama mzazi wa staa huyo wa Bongo aliwasihi wanamitandao kuepuka kumuingiza kwenye ugomvi na Zuchu huku akimtaja malkia wa Zanzibar kama bintiye.
“Wasinigombanishe na mwanangu Zuchu. Mimi sina ugomvi na mtu. Wasiniingize kwenye mambo hayo,” alisema.
Tetesi kuwa Mama Dangote anampendelea mpenzi wa zamani wa Diamond, Tanasha Donna badala ya Zuchu ziliibuka baada ya mwimbaji huyo wa Kenya kumsherehekea hivi majuzi kwa zawadi za gharama kubwa kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo ilipita takriban miezi miwili iliyopita.
Mama Dangote hata hivyo ameweka wazi kuwa huyo mzazi mwenza wa Diamond alimzawadi kwa niaba ya mtoto wake Naseeb Jr.