Mamake Diamond, Mama Dangote afurahishwa na vazi la ndoa la Zuchu

Mamake Diamond anaonekana kuwa na uhusiano mzuri na Zuchu.

Muhtasari

•Mama Dangote amekuwa akimzungumzia vyema Zuchu na kuonyesha upendo mkubwa kwake kupitia mitandao ya kijamii.

•Matendo ya hivi punde ya Mama Dangote yamepandisha tetesi kuwa huenda Diamond sio bosi wa Zuchu tu bali pia mpenziwe.

Image: INSTAGRAM// MAMA DANGOTE, ZUCHU

Mama ya staa wa Bongo Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote anaonekana kuwa na uhusiano mzuri na anayedaiwa kuwa mkwe wake mtarajiwa, Zuchu.

Katika siku za hivi majuzi, Mama Dangote amekuwa akimzungumzia vyema binti huyo na nguli wa taarab, Khadija Kopa na kuonyesha upendo mkubwa kwake kupitia mitandao ya kijamii.

Siku ya Jumanne, mamake Diamond alichapisha picha nzuri ya Zuchu akiwa amevalia gauni refu la kijani kibichi na kusema kuwa vazi hilo ni sahihi kwa ajili ya harusi ya Kiislamu.

"Zuchu... 💚👌🏼 Ndio Nguo ya ndoa kwa Waislamu," aliandika chini ya picha hiyo.

Posti hiyo ilikuja kabla ya chapisho lingine ambapo alikuwa akitangaza tamasha la Zuchu nchini Comoro lililopangwa kufanyika Januari 7, 2023.

Mama Dangote alitoa wito kwa Wacomoros kujitokeza kwa wingi kwenye shoo hiyo na kudokeza kwamba ataungana nao.

"Habari zenu wapenzi wa Comoro, nimefurahi sana kuwa miongoni mwenu tarehe 7 Januari, 2023 kwa ajili ya "TAMASHA LA MWAKA" pale Uwanja wa Malouzini kwa shoo ya kukumbukwa. Njooni wote tutaburudika. Karibuni Mendjiii #ZUCHUINCOMORO," aliandika.

Matendo ya hivi punde ya Mama Dangote yamepandisha tetesi kuwa huenda mwanawe Diamond sio bosi wa Zuchu tu bali pia mpenzi wake.

Mwezi uliopita hata hivyo, Diamond alijitokeza wazi na kukana kuchumbiana na Zuchu licha ya  wawili hao kunyoosha maelezo kuwa ni wapenzi hapo awali.

Diamond katika wimbo wake mpya wa Chitaki, kuna vesi moja ambayo anasikika akisema kuwa wanaosema anachumbiana na Zuchu ni wazushi tu ambao wanatafuta sababu ya kuendelea kumsema yeye na msanii huyo wake.

Katika kipande hicho cha wimbo huo ambapo anaonekana kama anamruka na kumsaliti Zuchu kimapenzi, anambembeleza mpenziwe mpya huku akimwambia kuwa maneno anayoyasikia kuwa anamvizia Zuchu si kweli hata kidogo.

“Wewe ndio mwisho wa reli, kwako naweka nukta. Waliokuambia natoka na Zuchu si kweli wanazusha. Wao ndio kazi yao sisi kutuhukumu…”  anasikika akiimba.

Tetesi za mahusiano kati ya wasanii hao wawili zimekuwa zikienezwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Matendo yao pamoja yakiwemo kubusu na kukumbatiana hadharani yamekuwa baadhi ya mambo ambayo mashabiki wametumia kufikia hitimisho kwamba wanatoka kimapenzi