Mapenzi matamu! Eudoxie ajigamba baada ya mpenziwe Grand P kuchorwa tattoo ya jina lake

Muhtasari

•Eudoxie amesherehekea kitendo hicho  na kubainisha kuwa mapenzi ambayo mumewe anampa ni matamu mno.

•Wawili hao walianza kuchumbiana zaidi ya miaka miwili iliyopita na wengi wamekuwa wakifuatilia mahusiano yao.

Image: FACEBOOK// EUDOXIE YAO

Mwanamuziki mbilikimo kutoka Guinea Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P amedhihirisha mahaba yake makubwa kwa mpenzi wake Eudoxie Yao kwa kuchorwa tattoo ya jina lake mkononi.

Grand P amepiga hatua kubwa ya kuchorwa "Love Eudoxie" kwenye kifundo cha mkono wake wa kushoto.

Eudoxie amesherehekea kitendo hicho  na kubainisha kuwa mapenzi ambayo mumewe anampa ni matamu mno.

"Nani ana mapenzi matamu kama haya? Mpenzi wangu Grand P," Eudoxie alisema kupitia Facebook.

Haya yanajiri takriban miezi miwili tu baada ya Grand P kumvisha mwanasoshalaiti huyo pete ya uchumba.

Mwanamuziki huyo mwenye maumbile ya kipekee alionekana akimuomba ndoa mpenzi huyo wake wa muda mrefu katika mojawapo ya vituo vya televisheni nchini Guinea.

Eudoxie Yao alifurahia hatua hiyo na kusema kuwa ana kazi kubwa ya kufanya katika kuafikia maamuzi ambayo hatayajutia mbeleni.

“Ombi la ndoa kutoka kwa mpenzi wangu wa zamani lilikuwa moto kweli kweli kwenye runinga moja kwa moja. Nina uamuzi mkubwa sana wa kuufanya… Bado naweza kumuamini kweli Grand P?” Mwanasoshalaiti huyo kutoka Ivory Coast alisema.

Grand P na Eudoxie wamekuwa kwenye mahusiano ya misimu kwa muda mrefu. Mara kwa mara wamekuwa wakikosana na kurudiana.

Wawili hao walianza kuchumbiana zaidi ya miaka miwili iliyopita na wengi wamekuwa wakifuatilia mahusiano yao hasa kutokana na utofauti mkubwa uliopo kati ya maumbile yao.