Marioo avunja kimya kuhusu kumuomba Diamond amsaini WCB

Marioo amepuuzilia mbali madai ya Diamond kuwa aliomba kujiunga na WCB.

Muhtasari

•Marioo amebainisha kuwa madai ya Diamond yalikuwa ni kuteleza kwa ulimi tu na kudai hayana ukweli wowote.

•Diamond akiwa kwenye mahojiano alidai kwamba Marioo alimfuata nyumbani kwake akiomba kusainiwa katika WCB.

Image: INSTAGRAM// MARIOO

Staa wa Bongo Omary Mwanga almaarufu Marioo amepuuzilia mbali madai ya bosi wa WCB Diamond Platnumz kuwa aliwahi kuomba kusainiwa kwenye lebo hiyo.

Marioo amebainisha kuwa madai ya Diamond yalikuwa ni kuteleza kwa ulimi tu na kudai hayana ukweli wowote.

Alikuwa akimjibu mtangazaji na mchekeshaji mashuhuri wa Bongo Mwijaku ambaye aliuliza ukweli kuhusu madai hayo.

"Ongea kitu mashabiki zako tupoe. Ulikosa nini mpaka uliomba kwenda UCHAFUNI? Tuambie tujirekebishe," Mwijaku alihoji chini ya chapisho moja la mwimbaji huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Marioo alijibu, "Hahaha Mkubwa kateleza, mfupa hauna ulimi😃."

Hapo awali, Diamond akiwa kwenye mahojiano alidai kwamba Marioo alimfuata nyumbani kwake akiomba kusainiwa katika WCB.

Diamond hata hivyo alimuonya mwimbaji huyo wa kibao 'Mi Amor' dhidi ya hatua hiyo akionya kuwa ingemletea madhara zaidi.

"Kabla ya kutoa Beer tamu Marioo alikuja nyumbani. Alipokuja na tukazungumza alitaka nimsaini. Nilimwambia, Marioo nikikutazama naona unafanya vizuri, nahisi kama kukusaini sio kukutendea  haki maana wewe tayari unafanya vizuri. Nikikusaini unajua kuna watu wengine ambao wataleta chuki zao kwa sababu unafuatana na Diamond na wasikupigie nyimbo. Kuna radio nyingi ambazo hazipigi nyimbo zangu, watakuwa hawakupigii zako," alisema.

Bosi huyo wa WCB alisema alimwagiza Marioo kutafakari kuhusu hatua hiyo na mazungumzo yao kabla ya kufanya uamuzi.

Aidha alisema kwamba aliahidi kumsaidia staa huyo wa Bongo katika matatizo yoyote aliyokuwa akipitia.

"Nilimwambia kama una matatizo aje ofisini tutampa hela.Tulizungumza vizuri na mdogo wangu Marioo akanielewa," alisema.

Diamond pia alibainisha kuwa uhusiano wake na Marioo ni mzuri na akafichua kwamba huwa wanakutana mara kwa mara.