Mchungaji Kiengei amsaidia Pritty Vishy kupata kazi za ubalozi baada ya kukutana, kusameheana

Mchungaji Ben Kiengei na mtayarishaji wa maudhui Pritty Vishy wamekutana na kusuluhisha mzozo wao.

Muhtasari

•Katika taarifa, mchungaji Kiengei alifichua kwamba baadaye aliwaalika wawekezaji kadhaa ambao walikubali kufanya kazi ya Pritty Vishy.

•Mkurugenzi Mtendaji wa Zunguka Africa Safaris, Samson Kimani alibainisha kuwa kipaji cha Pritty Vishy kinalingana na maono ya kampuni yake.

walikutana Jumatano mchana.
Pastor Ben, Pritty Vishy na mtangazaji Lizz Wangui walikutana Jumatano mchana.
Image: ZUNGUKA MEDIA

Siku ya Jumatano, Wakenya wawili mashuhuri ambao wamekuwa wakizozana kwa siku mbili zilizopita, mchungaji Benson Gathungu almaarufu ‘Kiengei’ na mtayarishaji wa maudhui Pritty Vishy walikutana kusuluhisha mzozo wao.

Wawili hao walikutana katika hoteli ya Triple O’S jijini Nairobi ambapo walifanya mazungumzo na kusameheana.

Katika taarifa, mchungaji Kiengei alifichua kwamba baadaye aliwaalika wawekezaji kadhaa ambao walikubali kufanya kazi ya Pritty Vishy.

“Prity Vishy ni mtu mzuri, msafi na mwenye roho nzuri ambaye alihitaji kukutana na mchungaji Ben, ingawa tumekutana katika hali isiyofaa, maisha mapya yameanza. Leo tumekaa kwenye mkutano na Pritty Vishy na Meneja wake Sharon Samba,” Kiengei alisema.

Aliongeza, “Baada ya kuzungumza, kusameheana pamoja na dada yangu Lizz Wangui Muchiri, niliwaalika wawekezaji fulani kwa sababu nimeona kwamba tunapaswa kumtumia Pritty na ushawishi wake kwa njia chanya ili kujenga na kubadilisha jinsi mambo yanavyofanya kazi katika maisha yake.”

Kufuatia mkutano huo wenye mafanikio, mtayarishaji maudhui huyo mwenye umri wa miaka 22 aliteuliwa kuwa balozi wa chapa ya kampuni ya utalii ya Zunguka Africa Safaris LTD, Fanikisha Micro Finance, Smartworld, Cactus Properties na JUJYS Mahogany Centre.

wakati wa mkutano wa Septemba 4, 2024.
Mchungaji Ben Kiengei na Mkurugenzi Mtendaji wa Zunguka Africa Safaris LTD Samson Kimani wakati wa mkutano wa Septemba 4, 2024.
Image: ZUNGUKA MEDIA

Akizungumzia kazi mpya la Pritty Vishy katika kampuni yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Zunguka Africa Safaris LTD Samson Kimani alielezea fahari yake kwa  jinsi mambo yalivyobadilika.

Alibainisha kuwa kipaji cha Pritty Vishy kinalingana na maono ya kampuni yake na akaeleza kuwa ana furaha na fahari kufanya kazi naye.

 "Zunguka tunaamini kuwa njia ya Mungu iko nje ya ufahamu wa mwanadamu, tulishuhudia jinsi maisha yalivyobadilika, na tunasimama kidete katika imani yetu kuwa anaweza kutumia njia yoyote kuleta mabadiliko.

 Tunajivunia na kufurahi kushirikiana na Pritty Vishy, ​​ambaye ushawishi wake wa ajabu na talanta ya kipekee inalingana kikamilifu na maono yetu. Kwa pamoja, tutatumia nguvu zake ili kuinua chapa yetu na kuendelea kuleta matokeo chanya,” Bw Kimani alisema.

Mapema wiki hii, Pritty Vishy alikuwa amezamia mtandaoni kumkashifu askofu Kiengei kwa maneno ya kuudhi aliyoyasema dhidi yake katika kipindi cha hivi majuzi cha televisheni.

Kiengei alikuwa ameomba msamaha mtandaoni, lakini mtayarishaji wa maudhui huyo mwenye umri wa miaka 22 mwanzoni alisita kumsamehe mtumishi wa Mungu.