"Mimi ni bilionea!" Ringtone Apoko afichua chanzo cha utajiri wake mkubwa

Apoko alijigamba kuwa utajiri wake mkubwa unatosha kuwafadhili wanamuziki wa wa Kenya

Muhtasari

•Apoko sasa ameweka wazi kuwa muziki wake ndio umefanikisha utajiri mkubwa ambao amejizolea kufikia sasa.

•Alijigamba kuwa utajiri wake mkubwa unatosha kuwafadhili wanamuziki wote wa muziki wa kutumbuiza wa Kenya.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Hatimaye mwanamuziki mashuhuri Ringtone Apoko amefafanua kuhusu chanzo cha utajiri wake mkubwa.

Kwa miaka mingi utajiri wa msanii huyo wa zamani wa nyimbo za injili umekuwa ukitiliwa shaka huku simulizi nyingi zikitolewa.

Apoko sasa ameweka wazi kuwa muziki wake ndio umefanikisha utajiri mkubwa ambao amejizolea kufikia sasa.

"Saa hii nimefikia bilioni. Mimi ni bilionea wa Kenya. Nilipata baada ya kuimba nyimbo za Mungu na nikatumia jina lake," Apoko alisema katika mahojiano ya simu na Mpasho.

Msanii huyo hata hivyo alibainisha kuwa mtu anahitaji "kutumia akili" ili aweze kuvuna vizuri kutoka kwa tasnia ya injili kama yeye.

"Kwa Mungu hufai kuenda ukisema asante pekee yake. Ukitaka chakula unafaa kuambia Mungu mara moja 'nataka chakula, nataka nyama, nataka kuku', lazima utoe maelezo, Mungu hupenda hivyo,"  Alisema.

Ringtone alipuuzilia mbali madai kuwa amejiunga na muziki wa kimapenzi kwa minajili ya manufaa ya kifedha.

Alijigamba kuwa utajiri wake mkubwa unatosha kuwafadhili wanamuziki wote wa muziki wa kutumbuiza wa Kenya.

"Mimi niko na pesa nyingi. Hata ninaweza kuifadhili tasnia ya muziki wa kidunia ya Kenya. Naweza kuwafadhili wote Siendi (kwa tasnia ya muziki wa kidunia) juu ya pesa," Ringtone alijibu kuhusu madai kwamba aligura injili ili kuwinda pesa.

Ringtone ni miongoni mwa wasanii wa Kenya wanaoaminika kuwa matajiri wakubwa zaidi na wenye mali ya thamani.

Kwa miaka mingi amekuwa akijiamba kuhusu utajiri wake huku akijiweka katika kiwango kimoja sawa na staa wa Bongo Diamond Platnumz

Takriban miezi mitatu iliyopita mwanamuziki huyo alichapisha orodha yake ya wasanii tajiri zaidi nchini Kenya.

Yeye mwenyewe ndiye aliyeongoza katika orodha hiyo yake iliyojumuisha wasanii kumi na wawili.

Katika orodha yake, Ringtone alidai kuwa anamiliki majumba matano ya kifahari katika maeneo ya Runda, Karen na Muthaiga.

Vile vile alisema  kuwa anamiliki magari saba ya kifahari yakiwemo Range Rovers, Mercedes -Maybach, BMW na kadhalika.

Akothee, Jaguar, Anerlisa Muigai, Khaligraph, KRG the Don, Betty Kyalo, Huddah Monroe, Otile Brown, DJ Moh na Size 8 ni baadhi ya wasanii wengine ambao alitambua utajiri wao