"Mimi sina uwezo!" Mpenzi wa ex wa Eric Omondi avunja kimya kuhusu madai ya kumpiga

Muhtasari

•Eric alimshtumu mjasiriamali huyo kwa kumpiga Chantal na kumsababishia majeraha mwilini baada ya kukataa kumfungulia mlango

•Traldi alibainisha kuwa mama yake alimfunza maadili mema na hata watu wa karibu naye wanafahamu hawezi kupiga mwanamke.

Nicola, Chantal na Eric Omondi
Nicola, Chantal na Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Ijumaa adhuhuri mchekeshaji maarufu Eric Omondi aliibua madai mazito dhidi ya mjasiriamali Nicola Traldi kupitia Instagram.

Bw Traldi ni mchumba wa sasa wa aliyekuwa mpenzi wa mchekeshaji huyo, Chantal Grazioli.

Eric alimshtumu mjasiriamali huyo kwa kumpiga Chantal na kumsababishia majeraha mwilini baada ya kukataa kumfungulia mlango. Alilaani kitendo hicho huku akisema kuwa ni ishara ya uoga na udhaifu.

"Mwanaume yeyote anayewekelekea mikono yake kwa mwanamke ni MUOGA!!! Nicola Traldi ni Muoga. Ni Dhaifu na Hajiamini. Nguvu za mwanaume huonyeshwa kikamilifu anapomlinda mwanamke na sio anampiga," Eric alisema.

Aliambatanisha ujumbe wake na video inayoonyesha akimsaidia mpenzi huyo wake wa zamani kutembea.

Katika video hiyo, Chantal alionekana akihangaika huku kukiwa na madoa ya damu kwenye miguu yake.

"Mbona upige mwanamke! Angalia alivyofanyia mguu wake! Hawezi kutembea," Eric alisikika akisema katika video hiyo.

Mchekeshaji huyo alitishia kuchukua hatua ya kisheria dhidi ya Traldi ili awe funzo kwa wanaume wanaowashambulia wanawake.

Traldi hata hivyo amejitokeza kukana madai ya kumpiga mpenzi huyo wake kupitia Instastori zake.

Huku akijitetea, Traldi alisema madai ya Eric si ya kweli huku akidai kuwa hana uwezo wa kupiga mwanamke. 

"Nimesingiziwa kwa jambo ambalo singefanya kamwe, lisilosemeka, Ni siku ya huzuni.. Nisingewekelea mikono yangu juu ya mwanamke. Mimi ni baba wa mabinti wawili. Ukweli utajulikana," Aliandika.

Aidha mjasiriamali huyo alibainisha kuwa mama yake alimfunza maadili mema na hata watu wa karibu naye wanafahamu hawezi kupiga mwanamke.

Traldi na Chantal walijitosa kwenye mahusiano baada ya malkia huyo mwenye asili ya Italia kutengana na Eric Omondi takriban miaka mitatu iliyopita.

Eric na Chantal waliotengana mwaka wa 2019 baada ya kuchumbiana kwa kipindi cha takriban miaka minne.