Mkewe Samidoh azungumzia kuwa marafiki na Karen Nyamu

Uhusiano wa Bi Nderitu na Karen Nyamu ni kama maji na mafuta.

Muhtasari

• Shabiki mmoja alimsihi mama huyo wa watoto watatu aweze kupatana na mzazi mwenzake Samidoh, Karen Nyamu.

•Edday ambaye alionekana wazi kutofurahishwa na maoni hayo alisema, "Kwani ni mimi namuoa."

Image: INSTAGRAM// EDDAY NDERITU, KAREN NYAMU

Mke wa mwimbaji wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, Edday Nderitu amejibu kuhusu kumaliza uhasama na seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu.

Wawili hao ambao wote wana watoto na Samidoh ni kama maji na mafuta na hata walihusika katika vita mapema mwezi uliopita  jijini Dubai 

Hivi majuzi, Bi Edday alichapisha video kwenye Tiktok na wanamitandao wakafurika chini yake kutoa maoni yao. Shabiki mmoja alimsihi mama huyo wa watoto watatu aweze kupatana na mzazi mwenzake Samidoh, Karen Nyamu.

"Penda bibi namba mbili kama wapenda Mungu,"  aliandika.

Edday ambaye alionekana wazi kutofurahishwa na maoni hayo alisema, "Kwani ni mimi namuoa."

Katikati mwa mwezi Desemba, Edday na Karen walihusika katika vita baada ya kukutana ana kwa ana kwenye eneo la burudani Dubai wakati Samidoh alikuwa anafanya tamasha la mwisho jijini humo.

Mzozo ulianza pale Karen alipoenda moja kwa moja hadi mahali Samidoh alikuwa ameketi na kukaa kwenye mapaja yake kwa nguvu.

Punde, Edday alisimama kutoka pale alipokuwa ameketi akaenda na kumshika mkono mumewe huku walinzi wakijaribu kuwatenganisha wanawake hao wawili. Kufuatia hilo, Samidoh alikabiliana na Karen.

Karen aliripotiwa kukasirika nusura ampige kofi mzazi huyo mwenzake kabla ya walinzi wake walipoingilia kati. Wakati huo, Edday alisimama na kujaribu kumnyakua Karen kutoka kwa mumewe kabla ya kuchukuliwa na walinzi.

Siku moja tu baada ya mzozo huo, Karen akiwa bado Dubai alitangaza kwamba ameamua kuachana na baba huyo wa wanawe wawili.

"Wanawake wakubwa na jasiri watathibitisha kwamba mara nyingi kiungo chetu dhaifu ni wanaume tunaojihusisha nao. Ninaacha mtindo huo.

Nimefanya uamuzi wa kusitisha uhusiano wangu na baba wa watoto wangu na sasa ni wa zamani." alisema

Nyamu aliandika zaidi kuwa hana majuto yoyote kuhusu kilichotokea Dubai, na kuahidi kuwa kisa hicho kilikuwa cha mwisho.

"Sitamani ningefanya mambo kwa njia tofauti," Nyamu alisema.

"Najua nilipaswa kumpigia simu na kumaliza kimya kimya, lakini niliamua kuiweka hadharani kama jinsi drama ilivyokuwa," alisema