Mpenziwe Baha azungumzia huzuni iliyomkumba baada ya kujifungua kabla ya wakati

Georgina amefichua kuwa ilimchukua takriban wiki nzima kulala pamoja na bintiye kwa mara ya kwanza.

Muhtasari

•Georgina amekiri kwamba alijawa na wasiwasi  alipofahamishwa kuwa angejifungua kabla ya wakati.

•Pia amefichua kuwa ilimchukua takriban wiki nzima kulala oamoja na binti yake Astra kwa mara ya kwanza.

Image: INSTAGRAM// TYLER MBAYA

MwanaYoutube Georgina Njenga amekiri kwamba alijawa na wasiwasi wakati  alipofahamishwa kuwa angejifungua kabla ya wakati.

Georgina ambaye ni mpenzi wa muigizaji Tyler Mbaya almaarufu Baha alijifungua mwezi Mei wakati akiwa na ujauzito  wa wiki 33. Ujauzito wa kawaida unapaswa kukaa kwa wiki 37 hadi wiki 42.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Georgina alisema alikuwa na hofu kubwa kuhusu matokeo ya mchakato wa kujifungua.

"Wakati huo nilichokuwa nawaza ni ikiwa mtoto atakuwa sawa kweli. Sikudhani mtu ata anaweza kujifungua kawaida akiwa na ujauzito wa wiki 33. Nilifikiri njia ya upasuaji ndiyo hutumika ikiwa unajifungua mapema. Nilikuwa nimechanganyikiwa. Hiyo wiki moja ambayo tulikuwa hospitali ndio wakati niliwahi kuchanganyikiwa zaidi maishani," Alisema.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 22 alijifungua mtoto wa kike mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mpenzi wake Baha.

Georgina hata hivyo amefichua kuwa ilimchukua takriban wiki nzima kulala pamoja na binti yake Astra kwa mara ya kwanza.

"Nilikuwa na hofu. Mtoto alikuwa kwa incubator. Vile mtu hujifungua alafu unalala na mtoto wako, mimi nililala na yeye kwa mara ya kwanza baada ya siku sita. Ilikuwa jambo la kuvunja moyo kukaona kwa incubator, kuona vile ni kadogo. Nilikahurumia," Alisema.

MwanaYouTube huyo alikiri kuwa wakati mwingine hata alijilaumu kwa masaibu yale bintiye alipitia baada ya kuzaliwa. 

"Nilijiuliza kwani ni wapi nilikosea wakati wa ujauzito wangu. Baada ya kufanya utafiti wangu nilibaini ni kawaida kwa  watu wanaojifungua wakiwa na umri mdogo," 

Takriban miezi miwili tayari imepita sasa tangu wakati kipusa huyo alipojifungua mtoto wake wa kwanza.

Georgina amefichua kuwa bintiye  amekuwa mtoto wa kawaida sasa na tayari ameongeza uzito wa mwili na kufikisha kilo 3.8.

Pia alifichua kuwa amekuwa akipata ushauri wa malezi kutoka kwa mama yake na pia kujifunza kupitia Youtube.