Mtoto wa pili? Mr Seed afunguka madai ya mkewe Nimo Gachuiri kuwa mjamzito

Seed alidokeza kwamba walipanga uzazi baada ya kujaliwa mtoto wa kwanza.

Muhtasari

•Katika mahojiano na Nicholas Kioko, msanii huyo alibainisha kuwa wakati wa wao kupata mtoto wa pili bado hujafika.

•Aliweka wazi kuwa hatakuwa na tatizo lolote endapo mtoto mwingine atapatikana kwa kuwa watoto ni baraka.

Mr Seed na mke wake Nimo Gachuiri
Image: INSTAGRAM// MR SEED

Mwimbaji wa nyimbo za injili na za mapenzi Mr Seed ametupilia mbali madai kuwa mke wake Nimo Gachuiri ni mjamzito.

Katika mahojiano na Nicholas Kioko, msanii huyo alibainisha kuwa wakati wa wao kupata mtoto wa pili bado hujafika.

Alisema kwamba kwa sasa yeye na mkewe wamejikita katika kulea mzaliwa wao wa kwanza, Gold Christen na kufanya kazi kwa ajili ya ustawi wao.

"Sio kweli, saa hii  ndio mtoto wetu mwingine anaingia shule. Kwenye mipango yetu tulikuwa tumesema angalau tupatie watoto nafasi na pia tujipatie nafasi ya kupambana," alisema.

Mwanamuziki huyo alibainisha kuwa ni bora kuchukua muda kabla ya kupata mtoto mwingine ili kutoa nafasi ya kumpa malezi bora.

Seed alisema kwamba alishtuka sana baada ya kuona ripoti zilizodai kwamba Nimo ni mjamzito huku akidokeza kwamba walichukua hatua za kupanga uzazi baada ya kumkaribisha mtoto wao wa kwanza ulimwenguni.

"Nilishtuka sana. Nilianza kujiuliza maswali nikakumbuka tuliona daktari miaka miwili iliyopita, nikauliza kwani imekwama?" alisema.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa hatakuwa na tatizo lolote endapo mtoto mwingine atapatikana kwa kuwa watoto ni baraka.

Seed zaidi alifichua kuwa mtoto wao wa kwanza anakaribia kujiunga na shule hivi karibuni na tayari wameanza mipango.

"Jana ndio tulikuwa tunapima sare yake ya shule. Yaani yeye kuingia tu shule, pesa nimelipa imesimamia karo ya masomo yangu yote maishani," alisema.

Alidokeza kuwa Gold Christen atajiunga na shule ya hadhi kwani nia yake ni kuwapa watoto wake maisha mazuri.

Mwimbaji huyo wa zamani wa  EMB Records na mchumba wake Nimo Gachuiri walijaliwa mtoto wao wa kiume, Gold Christen, mnamo  Machi 6, 2018.