Mulamwah akataa busu la kipusa aliyemlilia amuoe baada ya kumzawadi vinono (+video)

Mulamwah hata hivyo alikataa busu hilo na kucheka tu.

Muhtasari

•Katika bango hilo, mrembo huyo alibainisha kuwa ana sifa za kuwa mke na kumtaka Mulamwah afunge ndoa naye.

•Faith alinyoosha mikono yake kumkumbatia mpenzi huyo wa zamani wa Carrol Sonnie na hata kujitolea kumbusu.

Mulamwah akutana na Faith
Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah hatimaye amekutana na mwanadada aliyekiri kumtamani na kujitolea kuwa mke wake.

Picha ya Faith Vaati Musyoki almaarufu Zubeidah kutoka Ukambani akiwa ameshika bango lenye maandishi ya kukiri mapenzi mazito kwa mchekeshaji huyo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu.

Katika bango hilo, mrembo huyo alibainisha kuwa ana sifa za kuwa mke na kumtaka Mulamwah afunge ndoa naye.

"Nikikuona kwa picha sipati usingizi," aliandika na kuambatanisha na nambari yake ya simu ili mchekeshaji huyo kuwasiliana naye.

Mulamwah alikutana na mwanadada huyo siku ya Jumanne asubuhi na kuchapisha picha na video kadhaa za mkutano wao.

Hakuenda mkono wazi ila mikononi alikuwa amembebea simu aina ya Oppo na shilingi elfu kumi ambazo alimkabidhi.

"Hatimaye nilikutana naye, Faith Vaati Musyoki, mrembo na mcheshi. Nilimpa zawadi ya simu mpya kabisa na kakitu kiasi 10k kwa kunionyesha upendo, kitu ambacho huwa sipati mara kwa mara. Asante sana. Wacha tueneze upendo na uzuri kila wakati. Baraka ♥️," Mulamwah alisema kwenye Instagram.

Faith ambaye alionekana kushangazwa sana na zawadi za mchekeshaji huyo alishindwa kuficha furaha yake na kumshukuru kwa kitendo kizuri.

"Sikuwa natarajia hivi!" alisema.

Huku furaha kubwa ikiwa imeandikwa usoni mwake, mwanadada huyo alinyoosha mikono yake kumkumbatia mpenzi huyo wa zamani wa muigizaji Carrol Sonnie na hata kujitolea kumpa busu.

"Nimefurahi. Hata naweza mchum" alisema.

Mulamwah hata hivyo alikataa busu hilo na kucheka tu.

Faith alibainisha kuwa alipendezwa na zawadi za mchekeshaji huyo na hata kufichua kwamba hajawahi kutumia simu kubwa kama aliyopewa.