Mume wa Akothee, Omosh atoweka mitandaoni wakati uvumi wa ndoa kuvunjika ukikithiri

Akaunti ya Omosh ilikuwa na zaidi ya wafuasi 72,000 kabla ya kutoweka siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Saa chache baada ya Akothee kufunguka kuhusu hali yake, akaunti ya Instagram ya mumewe yenye wafuasi zaidi ya elfu sabini imetoweka.

•Badala ya jina 'Mrs Omosh', aliweka maelezo ya kazi zake. Hapo awali, alijitambulisha kama 'Mrs Shweizer' na 'Marketer'.(Muuzaji).

Akothee na mkewe Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Wasiwasi kuhusu hali ya ndoa ya Akothee na Denis ‘Omosh’ Shweizer umeendelea kupamba moto huku matukio ya hivi punde yakidokeza kuwa huenda kuna kitu kikubwa kinaendelea nyuma ya pazia.

Saa chache tu baada ya mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 kutoa taarifa ya kutia wasiwasi akifichua kwamba mambo hayajawa sawa kabisa katika maisha yake katika miezi michache iliyopita baada ya kupata ukweli fulani, akaunti ya Instagram ya mume wake yenye wafuasi zaidi ya elfu sabini imetoweka.

Akaunti ya Instagram ya Mister Omosh ilizimwa siku ya Jumanne na kuzidisha uvumi kwamba kunaweza kuwa na matatizo mahali fulani ambayo bado hayajafichuliwa. Akaunti hiyo ilikuwa na takriban wafuasi 72,000 kabla ya kutoweka. Hata hivyo, haijulikani ikiwa akaunti imezimwa kwa muda au kabisa.

Akothee tayari alikuwa ameacha kufollow akaunti hiyo kabla haijazimwa na pia alikuwa amefuta picha kadhaa za mume huyo wake mzungu.Mama huyo wa watoto watano pia alikuwa amefanya mabadiliko kadhaa kwenye akaunti yake ya Instagram, akiondoa jina 'Mrs Omosh' kutoka kwa wasifu wake.

Badala ya jina 'Mrs Omosh', aliweka maelezo ya kazi zake. Hapo awali, alijitambulisha kama 'Mrs Shweizer' na 'Marketer'.(Muuzaji).

Baada ya kufanya mabadiliko kwenye wasifu wake, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alijitambulisha kama Mkurugenzi Mtendaji AKOTHEE SAFARIS, Mkurugenzi Mtendaji AKOTHEE FOUNDATION na MSHAURI WA MASOKO. 

Akothee alibadilisha wasifu wake wa Instagram mwezi Aprili mwaka huu baada ya kufunga ndoa na Denis Shweizer katika harusi ya kifahari iliyofanyika jijini Nairobi. Wenzi hao walioonekana kuwa muungano mzuri sana walikuwa wameahidi harusi ya pili ambayo iliratibiwa kufanyika Uswizi lakini haikufanyika.

Mwanamuziki huyo alifunga ndoa rasmi na mzungu Dennis Shweizer katika harusi ya kufana ya kifahari iliyofanyika Aprili mwaka huu baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa. Haijabainika kama wawili hao bado wako pamoja kama mke na mume. Hata hivyo, wengi wamekuwa wakikisia kuwa ndoa hiyo tayari imevunjika.

Tetesi za kuachana zilianza miezi kadhaa iliyopita baada ya mwimbaji huyo kuacha kuonekana na mumewe sana kama ilivyokuwa kabla ya harusi yao na kwa muda mfupi baadaye. Tetesi hizo hata hivyo ziliongezeka baada ya Akothee kutoa taarifa akidokeza kuwa mambo hayajawa sawa na amekuwa akishiriki vipindi vya ushauri wa kisaikolojia na mtaalamu katika muda wa miezi miwili iliyopita.