"Mwanamke muovu sio mimi!" Nyamu ajibu madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh

Karen alidokeza kuwa pia yeye ni mama ambaye ana watoto na mwimbaji huyo.

Muhtasari

•Mwanamtandao alimwambia Bi Nyamu kuwa anatafuta laana tu na akamuonya kwamba anachofanya kitamuandama baadaye.

•Seneta huyo alibainisha kuwa yeye siye mwovu katika yote ambayo yamekuwa yakiendelea kama jinsi wengi wamekuwa wakidhani.

Karen Nyamu, Samidoh, Edday Nderitu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amejibu kwa hasira baada ya kushtumiwa kwa kuvunja ndoa ya mwimbaji wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Siku ya Ijumaa, mtumizi wa Instagram aliibua madai mazito kwamba mama huyo wa watoto watatu anafurahia kuvunja ndoa  ya mwanamuziki huyo ya zaidi ya mwongo mmoja na kumsababishia machozi mkewe Samidoh, Edday Nderitu.

@lin_njoks alimwambia Bi Nyamu kuwa anatafuta laana tu na akamuonya kwamba anachofanya kitamuandama baadaye.

"Wewe ni muovu Nyamu. Unafurahia kuvunja ndoa ya mtu mwingine. Siku moja utalipa. Kumbuka laana huwa kwa kizazi. Tahadhari wakati unalilisha mwanamke mwingine. Wakati wako unakjuja kuwa tayari kukabiliana na tukio kama hilo. Hii ni kukosa heshima sana," mwanamtandao huyo alimwandikia Karen.

Huku akijibu, seneta huyo alibainisha kuwa yeye siye mwovu katika yote ambayo yamekuwa yakiendelea kama jinsi wengi wamekuwa wakidhani.

Karen alidokeza kuwa pia yeye ni mama ambaye ana watoto na mwimbaji huyo.

"Hiyo ujinga yenyu kwani mimi si mwanamke na watoto wangu si watoto? Mwanamke muovu sio mimi," alisema.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya mkewe Samidoh, Edday Nderitu kumkashifu seneta huyo akimtaja kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake.

Ijumaa asubuhi, Edday alimpa onyo mumewe kuhusu uhusiano na Nyamu huku akimjulisha kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Edday alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Licha ya yote, anasema, amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya mwanamuziki huyo.

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"

Seneta  Karen Nyamu na  Samidoh walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla ya mazishi ya shemeji wa naibu rais Rigathi Gachagua, Nancy Muthoni katika eneo la Gatanga, kaunti ya Murang'a siku ya Alhamisi.

Baadaye jioni, Bi Nyamu alichapisha picha kadhaa  za hafla hiyo kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake, wakili huyo alibainisha kuwa alikuwa amehudhuria ili kufariji familia ya naibu rais.

Kati ya picha alizochapisha ni pamoja na moja ya mzazi mwenzake Samidoh akitoa hotuba yake kwenye hafla hiyo na nyingine inayoonyesha wakiwa wamekaa karibu na kuonekana kufurahia muda pamoja.