Mwandani wa Harmonize afichua mabadiliko ambayo Kajala atafanya Kondegang

Muhtasari

•Mwijaku ameweka wazi kuwa uhusiano wa kimapenzi kati ya Harmonize na Kajala hautaathiri utendakazi wao.

•Mwandani huyo wa Harmonize amesema kuwa Kajala ana uwezo mkubwa wa kufanya Kondegang kuwa bora zaidi.

Mwijaku
Mwijaku
Image: HISANI

Mtangazaji maarufu kutoka Tanzania Mwijaku ameeleza imani yake kwa Kajala kuwa CEO mpya wa timu ya usimamizi ya Konde Music Worldwide.

Mwandani huyo wa Harmonize amesema kuwa Kajala ana uwezo mkubwa wa kufanya Kondegang kuwa bora zaidi.

Ameeleza kuwa muigizaji huyo anastahili wadhfa aliopatiwa na Harmonize kwa historia yake katika tasnia ya burudani Tanzania ni ya kuvutia.

"Kajala anaingia pale kuongeza thamani. Ana utofauti mkubwa na wanawake wengine. Anakwenda kuchora njia Kondegang kuenda kimataifa zaidi," Mwijaku alisema alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari.

Mtangazaji huyo amewadokezea mashabiki mabadiliko mengi mazuri katika Kondegang katika muda wa miezi sita ijayo.

Ametoa hakikisho kuwa mpenzi huyo wa Harmonize ataleta utaratibu, uwajibikaji na urasimu katika Kondegang akihudumu kama CEO.

"Tumpe Kajala miezi sita, Kondegang itakuwa hatua ya juu zaidi katika tasnia ya burudani," Alisema.

Mwijaku pia aliweka wazi kuwa uhusiano wa kimapenzi kati ya Harmonize na Kajala hautaathiri utendakazi wao.

Hivi majuzi Harmonize alimteua Kajala kuwa meneja wake na CEO wa timu ya manejimenti ya Konde Music Worldwide baada ya kuzika ugomvi wao katika kaburi la sahau.

Meneja wake wa usanii Choppa TZ ndiye aliyetangaza habari za uteuzi wa Kajala huku akimkaribisha kwenye  timu yao.

"Niruhusu nimkaribishe katika timu ya usimamizi mkurugenzi na meneja mpya Frida Kajala. Nimefurahi kufanya kazi na wewe shem," Choppa alitangaza kupitia Instagram.

Kajala anaungana na Chopa, Mjerumani na Jose Wamipango katika timu ya usimamizi wa Harmonize na Konde Gang Music Worldwide.